WAWILI WAFUNGWA MIAKA 30 KWA UBAKAJI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 21 January 2026

WAWILI WAFUNGWA MIAKA 30 KWA UBAKAJI

 


Na Mwandishi wetu, Simanjiro


maipacarusha20@gmail.com


WAKAZI wawili wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka kwa zamu msichana mwenye umri wa miaka 24.


Pamoja na kumbaka na kumwingilia kinyume cha maumbile msichana huyo pia walimpora simu aina ya Samsung na kumwibia fedha zake Sh70,000.


Hata hivyo, katika hukumu ya kesi hiyo namba 10374/2025 iliyotolewa mji mdogo wa Orkesumet na hakimu wa mahakama ya wilaya hiyo Nicodemo washtakiwa watatu kati ya watano hawakuwepo mahakama hapo. 


Hakimu Nicodemo amewataja washtakiwa Meshack Paulo (23) na Ibrahim Ibu (24) ambao ni wachimbaji wa madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani walimbaka, kumlawiti msichana huyo


Amesema washtakiwa hao na wenzao watatu Februari 4, 2025 kwa pamoja walimbaka msichana huyo ambaye ni muhudumu wa bar ya Feri mwenye umri wa miaka 24.


Ameeleza kwamba wakati msichana huyo usiku huo wa saa 8 akitoka kazini akitembea kwenda nyumbani alimuona mshtakiwa wa kwanza Meshack akiwa na pikipiki kisha akampakiza.


Amesema alipakia pikipiki hiyo na walipofika na eneo la karibu na kanisa la Ngurumu ya Upako wakati akipelekwa nyumbani walisimamishwa na watu wengine wanne wakawa watano.


Ameeleza kwamba aliwatambua watu hao kutokana na mwanga wa nishati ya umeme iliyokuwa kwenye eneo la kanisa hilo wakaanza kumkaba.


Ameeleza kwamba katika ushahidi wake msichana huyo akadai kuwa mshtakiwa wa kwanza Meshack alimziba mdomo kisha wakambaka kwa zamu.


Amesema pia washtakiwa hao wakamnyang'anya simu aina ya Samsung yenye thamani ya Sh600,000 na fedha Sh70,000.


Katika utetezi wao mshtakiwa namba moja Meshack alikubali kuwa eneo la tukio ila hakushiriki ubakaji na mshtakiwa wa pili ameeleza kwamba hakuwepo kwenye tukio hilo.


Hata hivyo, hakimu Nicodemo akisoma hukumu hiyo ameeleza kwamba mahakama hiyo imewatia hatiani washtakiwa hao na kuwahukumu adhabu ya miaka 30 gerezani ili iwe funzo kwa watu wengine wenye tabia kama hizo


MWISHO

No comments: