LHRC na PALU waiomba serikali kurejea kuruhusu watu kuishitaki katika mahakama ya Afrika ya haki za Binaadamu na Watu - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 26 February 2026

LHRC na PALU waiomba serikali kurejea kuruhusu watu kuishitaki katika mahakama ya Afrika ya haki za Binaadamu na Watu




Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha sheria na Haki za Binaadamu(LHRC) Dr Wakili Anna Henga 

Mussa Juma,Maipac



Maipacarusha@gmail.com

Arusha. Serikali imeombwa kurejea kuruhusu watu binafsi au Asasi za kiraia kuishitaki katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu (ACHPR) yenye makao makuu yake jijini Arusha, ili kukuza masuala ya haki za binaadamu na Diplomasia ya kimataifa .



Mwaka 2019 Serikali ya Tanzania ilijiondoa katika itifaki kifungu cha 34(6) kinacho ruhusu wananchi na Asasi za kiraia kuishitaki kwa kile ambacho ilielezwa ni baada ya kubainika kuwepo kwa dosari katika maamuzi ya mahakama hiyo.



Wakizungumza na waandishi wa habari katika Kongamano la Wadau wa mahakama hiyo, ambalo linaendelea jijini Arusha, kabla ya kuanza vikao vya mahakama hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha sheria na Haki za Binaadamu(LHRC) Dr Wakili Anna Henga na Mtendaji Mkuu wa chama cha wanasheria wa Afrika (PALU), Wakili Donald Deya walisema haileti sura nzuri kimataifa kwa Tanzania kujiondoa kushitakiwa Arusha.


Dr Henga alisema kwa kuwa sasa Serikali inajitahidi sana kurejesha diplomasia yake kimataifa ni wakati muafaka kurejea katika mahakama hiyo.


Dr Henga ambaye alikuwa mmoja wa wazungumzaji katika Kongamano hilo alisema, Tanzania licha ya kujitoa imekuwa ikitekeleza baadhi ya hukumu zilizotolewa na mahakama hiyo.


"Kuna maamuzi ya kesi ya uchaguzi yaliyotolewa na mahakama hiyo, kutaka wakurugenzi waondolewe kusimamia uchaguzi serikali imetekeleza japo si kwa mambo yote lakini walau kuna hatua zimechukuliwa ya kuondolewa wakurugenzi"alisema


Alisema kwa sasa Watanzania wanaotaka kufungua kesi wanalazimika kupeleka kesi zao kwanza tume ya haki za binaadamu na watu Banjuu nchini Gambia na ndipo kesi iletwe Arusha jambo ambalo wananchi wengi hawawezi.


Akiendesha mjadala kuhusu utelelezwaji wa maamuzi ya mahakama hiyo kwa nchi za Afrika, Dr Henga alisema miaka 20 ya mahakama hiyo kuna maamuzi ambayo yametolewa na kutekelezwa na nchi 34 za Afrika ambazo ni wanachama wa mahakama hiyo.

Kwa upande wake, Wakili Deya alisema haoni sababu za msingi za Tanzania kuendelea kuzuia kushitakiwa kwani hoja kuwa maamuzi ya mahakama hiyo yalikuwa yakikiuka Katiba ya Tanzania sio sahihi.


"Maamuzi ya kesi nyingi yaliyotolewa hayatofautiani na maamuzi ya mahakama za ndani ya Tanzania na vyombo vingine vya umoja wa mataifa hivyo hakuna dosari"alisema


Hata hivyo Deya alisema wanaimani serikalo ya Rais Samia Suluhu itakamilisha mchakato wa kurejea katika mahakama hiyo hivi karibuni.


Deya ambaye ni mmoja wa mawakili wa kesi zaidi ya 20 ambazo zimefunguliwa katika mahakama hiyo na Watanzania, alisema kimsingi kesi nyingi ambazo zimefunguliwa ni za wafungwa ambao wanaamini hawakutendewa haki na mahakama za ndani Tanzania.


Wakili Deya alisema pia kesi nyingine ni za kisiasa ambazo, baadhi tayari zimetolewa maamuzi na serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya maboresho katika sheria zake.


Mnamo Novemba 24 mwaka 2022 akifungua mkutano wa 27 wa chama cha Mawakili Afrika ya Mashariki(EALS) jana jijini Arusha, Rais Samia Suluhu alisema Tanzania imejiondoa kwa muda katika mahakama hiyo, kutokana na uwepo wa changamoto ambazo zitapatiwa ufumbuzi.


Alisema katika mahakama hiyo ambayo makao makuu yake yapo jijini Arusha, Tanzania ilikuwa inaongoza kwa kuwa na kesi nyingi, ambapo kati ya kesi 3060 ambazo zilikuwa zimeandikishwa Tanzania pekee ilikuwa na kesi zinazofikia 270.


Mahakama ya Afrika ya haki za binaadamu za watu, yenye makao makuu yake jijini Arusha, ilianzishwa mwaka 2004 kutokana na maazimio ya Umoja wa nchi huru za Afrika mwaka 1998.

Mwisho.












No comments: