![]() |
Na Mwandishi wetu, Mirerani
maipacarusha20@gmail.com
CHAMA cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) kinafanya mkutano mkuu wake wa mwaka kwa muda wa siku mbili katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.
Mwenyekiti wa MAREMA Elisha Nelson Mnyawi amewapongeza viongozi hao wa wachimbaji kwa kukutana na kufanya mkutano wao ili kuzungumzia mafanikio na changamoto zao.
Elisha Mnyawi ameeleza kwamba kupitia mkutano mkuu wa wachimbaji hao ndiyo wanaweza kuzungumza na kupitisha mambo mbalimbali yanayowahusu.
Amewapongeza viongozi hao wa wachimbaji kwa kupitisha tamko la kila mchimbaji kuchangia MAREMA Tawi asilimia moja ya mazao ya mapato yake pindi akipata uzalishaji ili kutunisha mfuko wao wenyewe.
"Nawashukuru kwa kuja kwani siku ya kwanza ya mkutano wetu umeenda vyema watu wa Benki ya NMB, CRDB na TANESCO wametupa elimu, kesho siku ya pili kutakuwa na mambo mengi na mgeni rasmi tunatarajia atakuwa Mhe RC wetu Queen Sendiga," amesema.
Amewashukuru viongozi hao kwa kupanga kufanya mkutano mkuu maalum wa marekebisho ya katiba yao ifikapo Machi 10 mwaka 2026 mjini Babati, ili kuiboresha zaidi.
Mgeni rasmi wa mkutano mkuu huo wa siku ya kwanza, Afisa madini mkazi Mirerani RMO George Kaseza amesema sekta ya madini inazidi kukua na kuzalisha matajiri wapya hapa nchini kupitia kauli mbiu ya madini ni utajiri na maisha 2030.
"Pamoja na hayo kila mchimbaji anapaswa kuandaa mpango wa uwajibikaji kwa jamii CSR, kwani unaweza hata kupanga kutoa shilingi milioni 4 kwa mwaka kwa awamu nne kupitia miradi ya maendeleo kwenye vijiji," amesema Kaseza.
Afisa madini mkazi Manyara, RMO Godfrey Nyanda amesema wachimbaji wa Babati, Kiteto, Mbulu na Hanang wamechangia shilingi milioni 500 kwenye pato la nchi kupitia madini yao.
Nyanda amewapongeza wachimbaji hao kwa namna ambavyo wamekuwa wakishirikiana na serikali pindi wakiwa na changamoto zinazowakabili.
Katibu mkuu wa MAREMA Tariq James Kibwe ameeleza kwamba miongoni mwa mafanikio ya mkutano mkuu huo ni kuboresha nafasi za viongozi wa matawi kuwa wilaya.
"Hivi sasa viongozi wa matawi watatambulika kiwilaya kupitia matawi ya awali ya Mirerani, Kiteto, Mbulu, Kastam Losinyai, Nadonyukini, Msitu wa Tembo, Magugu na Magara Babati," amesema.
Amesema pia MAREMA Mkoa na Wilaya wameongeza kamati mbalimbali ikiwemo kamati ya usuluhishi na migogoro, kamati ya miradi na uchumi na kamati ya vijana, kama ilivyo kwenye shirikisho la vyama vya wachimbaji madini Tanzania (FEMATA).
MWISHO

No comments:
Post a Comment