OFISI YA AG MKOA WA MTWARA YASHIRIKI SIKU YA SHERIA NCHINI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 2 February 2026

OFISI YA AG MKOA WA MTWARA YASHIRIKI SIKU YA SHERIA NCHINI

 




Na mwandishi wetu


maipacarusha20@gmail.com


Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mtwara, imeungana na wadau wa sheria nchini kushiriki siku ya sheria iliyoadhimishwa kitaifa leo tarehe 2 Februari 2026.


Siku ya sheria katika mkoa wa Mtwara, imeadhimshwa kwenye  viwanja vya Mahakama Kuu Mkoa wa Mtwara na kuongozwa na Mhe.Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Mtwara Edwin Kakolaki.



Akitoa salam za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Wakili Nunu Mangu amesema kuwa ustawi na maendeleo ya Jamii na Taifa lolote lile Duniani huletwa na mihimuli mitatu ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama.


Wakili Nunu Mangu, ambaye ni Mwanasheria kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mtwara, ameeleza kuwa Mahakama ni mlezi wa katiba, mlinzi wa haki za binadam, utawala wa sheria na  nguzo muhimu katika kukuza na kuendeleza ustawi wa maendeleo ya Taifa.



Katika hotuba yake Mhe.Jaji Edwin Kakolaki ameeleza kuwa Mahakama itaendelea kusimamia haki kufikia malengo ya dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili kuongeza na kudumisha imani ya wananchi kwa mahakama.


Amesema kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaongelea utawala bora na haki kama kipaombele muhimu katika kufikia maendeleo ya Taifa, hivyo mahakama itaendelea kutoa haki kwa wananchi wote bila upendeleo.


Akitoa salam za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala, amesema utoaji wa haki mapema kwa wananchi, kutadumisha amani na mshikamano wa Taifa sambamba na kukuza uchumi kwa mtu mmojammoja na Taifa.


"Nchi yenye amani na utulivu, inakaribisha wawekezaji na kuiletea maendeleo, nitoe rai kwa wadau wote wa haki na madai, kutoa haki mapema na bila kuchelewesha" amesema Kanali Sawala.


Naye Lightness Kikao, Makamu Mwenyekiti TLS Mkoa wa Mtwara, amesisitiza juu ya kuendelea kufuatwa kwa utawala wa sheria nchini, ili kufanya wananchi waendelee kuiamini mahakama.



No comments: