![]() |
| Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama |
Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro linafanya uchunguzi wa tukio la ajali ya magari mawili ya mizigo kugongana na kusababisha vifo vya watu watatu wakiwemi madereva wa magari hayo
Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Alex Mkama alisema kuwa tukio hilo limetokea Febduari 25, 2026 saa nane usiku katika eneo la Maseyu, kata ya Gwata, Wilaya ya Morogoro.
Kamanda huyo alisema magari mawili yenye shehena ya mbao na mafuta yakiwa katika uelekeo tofauti katika barabara ya Morogoro - Dar es Salaam yaligongana na kusababisha vifo vya madereva wote wawili na mtu mwingine anayedhaniwa kuwa ni utingo.
Aidha alisema gari lenye shehena ya mbao likitokea mkoani Morogoro kwenda Dar es Salaam likiendeshwa na dereva ambaye hajafahamika jina, liliacha njia yake na kulifuata gari ambalo lilikuwa na shehena ya mafuta ambalo lilikuwa linatokea Dar es Salaam kuelekea Morogoro na kugongana kisha kuwaka moto na kuteketea.
Jeshi la zimamoto na uokoaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wamejitahidi kuudhibiti moto huo na kufanya upekuzi kwenye magari yote mawili na kufanikiwa kupata mabaki ya miili miwili kwenye gari lenye shehena ya mafuta na mwili mmoja kwenye gari lenye shehena ya mbao.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni uzembe wa aliyekuwa dereva wa gari lenye shehena ya mbao kuacha upande wake na kulifuata gari lenye shehena ya mafuta.
Akisema uchunguzi zaidi wa tukio unaendelea ili kubaini anuani kamili za magari, umiliki na utambuzi wa miili iliyookolewa eneo la ajali.
Alisema jeshi la Polisi linaendelea kuwakumbusha watumiaji wote wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na madhara yake.
Mwisho
.jpg)
No comments:
Post a Comment