![]() |
| Mhandisi Anitha James,Kaimu Mratibu wa Kitaifa programu ya BBT |
![]() |
| Mkurugenzi msaidizi Mipango na Bajeti wa Wizara ya Kilimo, Mohamed Chikawe |
Na Lilian Kasenene,Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
POGRAMU ya Jenga Kesho iliyo bora (BBT) imeanza kushuka ngazi za Halmashauri za wilaya ili kuwafikia vijana wengi zaidi vijijini na mijini.
KAIMU mratibu wa Kitaifa wa Programu hiyo ya BBT, Mhandisi Anitha James, alieleza hayo mjini Morogoro wakati akizungumza na wadau wa mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayofanya kazi na Vijana katika sekta ya Kilimo, waliofadhiliwa na shirika la kimataifa la AGRA.
Alisema programu imeanza mwaka wa fedha 2025/2026, na hatua hiyo inalenga kuongeza uzalishaji, ajira na ushindani wa kilimo baada ya mafanikio kwenye mashamba ya mfano ya Chinangali na Ndogowe yaliyopo mkoani Dodoma.
“Kwa sasa tumeanza na halmashauri 20 katika mikoa 10 ya Dodoma, Singida, Tabora, Kagera, Mara, Njombe, Geita, Mbeya, Pwani na Katavi na baadhi ya halmashauri zimeshaanza udahili,"alisema Kaimu mratibu huyo wa Kitaifa wa BBT
Akasema halmashauri ya Muleba Mkoa wa Kagera pekee imeshadahili vijana zaidi ya 282 kwaajili ya kilimo cha mpunga huku Kaliua mkoani Tabora wakidahili vijana zaidi ya 300 kwaajili ya kilimo cha kahawa.
.
Akasema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali,wadau wa maendeleo na sekta binafsi ambapo lengo ni kuwafikia vijana zaidi ya 10,000 ifikapo 2030, lengo likiwa kuhakikisha kila kijana anapata nafasi ya kushiriki katika kilimo cha kisasa na chenye tija.
Kaimu Mratibu huyo alisema tangu programu hiyo kuanza 2022 na kuzinduliwa rasmi na Rais Mhe Samia Suluhu Hassan mwaka 2023, wameweza kutoa mikopo ya thamani ya zaidi ya shilingi milioni 600 kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Kuhusu uongezaji thamani ya mazao,Anitha alisema kwa kushirikiana na bodi ya Mkonge wamedahili vijana 300 na kuwapatia mafunzo, kuwawezesha upatikanaji malighafi na kutengeneza bidhaa za kiutalii ambazo zimeendelea kuuzwa katika masoko mbalimbali.
Aidha kwa kushirikiana na bodi ya Korosho, akasema wametoa mitambo ya kubangua korosho na kwa kushirikiana na sekta binafsi tayari wamezifikia halmashauri za wilaya za Mkuranga mkoani Pwani na Mtwara.
Kaimu mratibu huyo wa BBT taifa akasema pia wameangalia kwa kipekee eneo la vijana kutoa huduma za ughani ambapo Vijana zaidi ya 1,240 katika kipindi cha kuanzia 2024 na wameendelea kufanya hivyo kwenye bodi ya Pamba, Korosho na katika kilimo cha zao la parachichi.
"Kwenye korosho huduma za ughani zimewezesha uzalishaji kuongezeka kutoka tani 100 kufikia 500 hivi sasa "Aliongeza.
Mkurugenzi msaidizi Mipango na Bajeti wa Wizara ya Kilimo, Mohamed Chikawe, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alisema Serikali imewekeza katika mitambo ya umwagiliaji, visima na mashine za usindikaji ili kupunguza changamoto zinazowakabili vijana.
“BBT imekuwa chachu ya mapinduzi ya kilimo cha vijana, imeongeza mnyororo wa thamani, masoko, mitaji na fursa zaidi. changamoto za mitaji, ardhi na uduni wa teknolojia ndizo zilizotufanya kuanzisha BBT ili vijana washiriki kikamilifu kwenye kilimo,” alisema Chikawe.
Aidha, wadau wa sekta binafsi, kwa nyakati tofauti akiwemo Baraka Chambua kutoka New hope community development organizations na Edfin Tongora, wa Shambani Consultants solution waliipongeza Serikali kwa kushusha programu hiyo hadi ngazi za chini, wakisema hatua hiyo itaongeza ushiriki mkubwa wa vijana na wanawake katika sekta ya kilimo
Walisema kushuka kwa BBT hadi ngazi za halmashauri kumeimarisha uratibu, takwimu sahihi na mazingira wezeshi kwa vijana kuendesha biashara zao.
Waliongeza kuwa kupitia ushirikiano wa Serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi ili kuwafikia vijana zaidi ya 10,000 ifikapo mwaka 2030.
Mwisho.


No comments:
Post a Comment