Na Pamela Mollel,Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua madhubuti kuimarisha sekta ya hifadhi ya jamii nchini, hatua inayolenga kuongeza ustawi wa wastaafu na watumishi wa umma kwa ujumla.
Akizungumza Februari 9, 2026 jijini Arusha katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Mheshimiwa Deus Clement Sangu, alisema Serikali imelipa kiasi kikubwa cha deni la michango lililorithiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kabla ya mwaka 1999.
Alieleza kuwa kati ya Shilingi Trilioni 4.46 za deni lililotambuliwa, tayari Shilingi Trilioni 4.26 zimelipwa, sawa na asilimia 95, huku taratibu za kuhakiki kiasi kilichosalia zikiendelea kabla ya kukamilisha malipo yote.
![]() |
| Wastaafu |
Kwa mujibu wa Waziri Sangu, hatua hiyo imeuongezea mfuko uimara wa kifedha na kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama. Hivi sasa, mafao yanalipwa ndani ya siku 30 tangu kukamilika kwa taratibu, huku pensheni zikianza kulipwa kila ifikapo tarehe 25 ya mwezi.
Aidha, maboresho ya mifumo ya TEHAMA yamerahisisha uhakiki wa wastaafu kwa njia ya kidijitali, jambo lililopunguza adha ya kusafiri mara kwa mara kufuata huduma ofisini.
Katika kuendeleza ustawi wa wastaafu, Serikali pia imepandisha kima cha chini cha pensheni kutoka Shilingi 100,000 hadi 250,000 kwa mwezi kuanzia Julai 2025, hatua inayolenga kuboresha maisha ya wastaafu nchini.
Tangu mwaka 2018, Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kinga ya jamii, ikiwemo kuunganisha mifuko ya pensheni na kubakiza miwili — PSSSF kwa sekta ya umma na NSSF kwa sekta binafsi — ili kuongeza ufanisi wa huduma na ulipaji wa mafao.
![]() |
| Waka |
Vilevile, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeendelea kutoa fidia kwa wafanyakazi wanaopata madhara kazini, huku Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ukiendelea kuboresha huduma za matibabu kwa wanachama wake.
Hatua hizi zinaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha mifumo ya hifadhi ya jamii inakuwa imara, jumuishi na yenye kumlinda mwananchi kuanzia akiwa kazini hadi anapostaafu.




No comments:
Post a Comment