Mwandishi wetu,Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Waandishi wa habari Kanda ya Kaskazini na kati, wamekubaliana kuandika uchunguzi wa uvamizi njia za wanyamapori (Shoroba) na athari za mabadiliko tabianchi nchini.
Mapito mengi ya wanyama nchini ikiwepo ya Kwakuchinja yaliyopo katikati ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Manyara yanaendelea kuvamiwa na watu kwa ajili ya shughuli za kibinadamu na kuathiri wanyamapori kuhama na biolojia yao.
Mabadiliko ya tabia nchi yanayochangiwa na uharibifu wa mazingira yameanza kusababisha kumezwa ardhi maeneo kadhaa ikiwepo eneo la pangani mkoani Tanga na ukame maeneo mengi nchini ikiwepo ya jamii za asili na kupungua barafu mlima Kilimanjaro.
Maamuzi ya kufanya uchunguzi huo yalifikiwa katika mafunzo ya uandishi wa habari za mazingira yaliyoandaliwa na mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu (THRDC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Waandishi wa habari ya kusaidia jamii za Asili (MAIPAC) kwa udhamini wa shirika la Umoja wa Mataifa la UNESCO.
![]() |
| Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma |
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma alisema kupitia mradi huo wanahabari ambao wanania ya dhati kufanya uchunguzi wa habari za mazingira watasaidiwa mahitaji kadhaa ikiwepo kupata msaada wa kisheria na kukutana na watendaji wa serikali na wataalam.
"Kuna mambo mengi mnaweza kuandika na kuleta mabadiliko katika jamii,Uwajibikaji na kuleta maboresho ya Sheria na sera za mazingira, hivyo MAIPAC na THRDC tutawapa ushirikiano"alisema Musa Juma
Alisema kila kukicha ushoroba wa kwakuchinja unaendelea kuzimwa, Ukame umeongezeka, hali joto na kuna maeneo yanamezwa na maji ikiwepo Pangaji mkoani Tanga, licha ya serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi bado watu wanakata miti kwa ajili ya mkaa nendeni mkachunguze nini kifanyike kuzuia"alisema
![]() |
| Mkuu wa Dawati za utetezi THRDC, Wakili Paulo Kisabo |
Mkuu wa Dawati za utetezi THRDC, Wakili Paulo Kisabo alisema THRDC itaendelea kutoa msaada na ushauri wa kisheria kwa wanahabari wa mazingira watakapohitaji.
"Sisi tupo pamoja na nyinyi kama kuna sheria unahiji ufahamu tujulishe na kama kuna changamoto za kisheria wakati wa kutimiza wajibu wako tujulishe kwani lengo ni kuhakikisha kunakuwepo mazingira bora ya kuishi watu "alisema wakili Kisabo
Kisabo alisema, wanahabari wanapaswa kuzijua sheria mbalimbali katika tasnia yao ili kufanyakazi vizuri lakini pia kufanyakazi kwa kuzingatia usalama wao na maadili.
Mkurugenzi wa Klabu za waandishi wa habari Tanzania(UTPC), Kenneth Simbaya aliwataka wanahabari kutimiza wajibu wao katika jamii kwa kuandika matatizo ya watu na suluhu yake badala ya habari za kupongezana tu.
Alisema imani ya wananchi kwa vyombo vya habari imeshuka kutokana na vyombo hivyo kutoandika mambo mengi yanayolalamikiwa na watu waliowengi hivyo lazima imani irejeshwe.
"Tunawashukuru MAIPAC na THRDC kuja na mradi huu sasa tuutumie kusaidia jamii, tuandike habari za kuleta suluhu ya changamoto za kimazingira za watu, tuzingatie maadili ya uandishi na tuongeze ubunifu katika habari zetu"alisema Keneth Simbaya
Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa Arusha, Claud Gwandu na Wanahabari Burhani Yakoub wa Tanga na Baraka Ole Moita wa Simanjiro, walikiri kuna changamoto za kimazingira katika maeneo mengi na kupitia mafunzo haya wanakwenda kuzifanyia kazi.
Mafunzo hayo yalishirikisha wanahabari za mazingira 35 kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dodoma, Manyara na Singida na yanatarajiwa kuendelea katika kanda zingine nchini.
Mwisho



No comments:
Post a Comment