![]() |
![]() |
| Wakili Paul Kisabo Akitoa mada kuhusiana na masuala ya ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari za mazingira jijini Arusha. |
Mwandishi wetu,Arusha
maipacarusha20@gmail.com
Waandishi wa habari za Mazingira Kanda ya Kaskazini na Kati, wametakiwa kuandika habari za uchunguzi ambazo zinachochea mabadiliko ya sheria na sera na kuhimiza uwajibikaji.
Wakitoa mada katika mafunzo ya waandishi wa habari za mazingira, yaliyoandaliwa na Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu (THRDC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari inayosaidia jamii za asili (MAIPAC), Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC), Kenneth Simbaya na Mkurugenzi wa MAIPAC, Mussa Juma walisema wakati wa kuandika habari za matukio umepita.
Simbaya alisema katika uandishi wa kisasa ni muhimu sana, habari ichochee mabadiliko ya sera na sheria badala ya kuandika matukio ya kila siku.
"LHRC na MAIPAC wameandaa mafunzo haya, ili muandike habari za uchunguzi za mazingira ambazo zinachochea mabadiliko lakini pia mzingatie maadili"alisema
Kwa Upande wake Juma, licha ya kuhimiza habari za uchunguzi ambazo zinaleta uwajibikaji katika jamii, aliwataka wanahabari kuzingatia maadili, mila na Tamaduni katika uandishi wa habari za mazingira.
"Tuandike habari ambazo zinaonesha mapungufu ya sera, kanuni na sheria, lakini pia habari ambazo zinaongeza ushiriki wa watu wengi kusoma na kufanya maamuzi"alisema
Akitoa mada kuhusiana na uandishi kwa jamii za Asili, aliwataka wanahabari kuzingatia mila na tamaduni zao, kuheshimu viongozi wa mila, kutoandika habari bila kupata idhini ya mtu ama jamii.
"kumeibuka tabia ya watu kwenda kwenye maeneo ya jamii za asili kama Wahadzabe kuwapiga picha na kuandika mambo bila jamii hiyo kuridhia ama kuwa na uelewa"alisema
Alisema katika uandishi wa habari za jamii za asili ni muhimu sana, kuheshimu mila zao, kutotumia lugha za kuwadhalilisha ama kuwa kera lakini muhimu pia kuwapa fursa wao kujieleza"alisema
Juma alisema katika mafunzo hayo, wanatarajia wanahabari kwenda kuchunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa jamii za pembezoni lakini pia migogoro ya ardhi ambayo imeanza kuibuka.
![]() |
Akitoa mada kuhusiana na masuala ya ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari za mazingira, Wakili Paul Kisabo aliwataka wanahabari kabla ya kwenda kuandika habari, kufanya tathmini za kiusalama na kuchukuwa tahadhari.
Wakili Kisabo pia alianisha sheria mbali mbali za habari na mazingira ambazo wanahabari wanapaswa kuzijua na kuzitumia katika utendaji kazi.
Waandishi wa habari 35 kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Singida, Dodoma na Manyara walishiriki mafunzo hayo ambayo yanadhaminiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Utamaduni na Elimu(UNESCO) ambapo mafunzo hayo pia yanatarajiwa kufanyika katika Kanda ya Ziwa, Kanda ya Mashariki na Pwani na Zanzibar.
![]() |






No comments:
Post a Comment