WACHEZAJI EUNICE NA MICHAEL WAIBUKA KIDEDEA KUJIZOLEA TUZO ZA TFS - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 24 February 2026

WACHEZAJI EUNICE NA MICHAEL WAIBUKA KIDEDEA KUJIZOLEA TUZO ZA TFS








Na Lilian Kasenene, Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com


MICHUANO iliyoendeshwa na wakala wa huduma za Misitu nchini (TFS) imemalizika katika viwanja vya Highland mjini Morogoro, wachezaji Eunice Makondo kutoka Kanda ya kati na Michael Kalay wa kanda ya kusini wakijizolea tuzo za kutosha kwa kuibuka vinara wa mbio ndefu.


Hafla ya kukabidhi tuzo hizo imefanyika siku Moja baada ya michuano hiyo iliyoshirikisha Michezo mbalimbali ikiwemo Riadha, za Mita 100, 200, 400, 800, 1,500, 3000 na 5,000 kwa upande wa wanawake na wanaume,mpira wa miguu, netball, karata, darts, Bao,Karata na Michezo mingine.


Tuzo kwa washindi zimekabidhiwa katika Kituo cha Mikutano cha Cate mjini Morogoro na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas.


Mchezaji Eunice Makondo (23) aliibuka kidedea kwa kujinyakulia tuzo Tano ikiwemo kinara kwenye ukimbiaji wa mbio ndefu za Mita 200,800,1500 na mita 3000 kwa wanawake pamoja na nafasi ya pili mbio za mita 100 na kupata medali sambamba na kikombe katika nafasi ya mshambuliaji bora kwa upande wa mpira wa pete.


Eunice kabla ya kupata Kazi TFS alisema amewahi kushindana kwenye michuano ya mbio na kuwa nafasi ya kwanza kwenye mashindano ya mbio ya Nyamongo, Serengeti mkoani Mara.


"Mimi Siri ya ushindi ni mazoezi, usisubiri mashindano, na huwa tunapata muda wa mazoezi ambao tumetengewa na ofisi, lakini jumamosi na jumapili pia, mazoezi ni afya, Mimi wananiita chembamba lakini yote haya ni kwa sababu nauweka sawa mwili wangu kwa mazoezi,"alisema Eunice.


Naye mchezaji Michael Karay kutoka Kanda ya Kusini aliibuka mshindi kwa kujizolea medali tatu kwa kushinda mbio za Mita 800,1500 na 5000 kwa wanaume.


Karay alitoa wito kwa wafanyakazi hususani wa Mamlaka hiyo kutenga muda kwaajili ya Mazoezi na kwamba amekuwa akishiriki michuano mbalimbali kila inapojitokeza hivyo kumfanya kuwa fit wakati wote.


Katibu Mkuu Dk Abbas alisema Wizara hiyo iko mbioni kuandaa michuano dhidi ya taasisi zake ili kuendeleza ukaribu na mashirikiano na kuwafanya watumishi kuendelea kuwa vizuri Kazini.


"Najua kuna wengine umri umekwenda, watakuwa nao na Michezo Yao, tutaanzisha bonanza kubwa ngazi ya Wizara kwa kushirikisha taasisi zake zote zilizopo"alisema Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Maliasili na Utalii.


Katibu mkuu huyo pia aliahidi zawadi ya shilingi milioni 1 kwa kila mchezaji aliyejizolea tuzo zaidi ya tatu katika Michezo hiyo.


Mwisho.

No comments: