Burhani Yakub,Tanga.
Kuporomoka kwa maadili ya vijana ikiwamo kukithuri kwa ngoma za usiku maarufu vigodoro na vijamvi katika maeneo mbalimbali mkoani Tanga kumewaibua wanawake wa kiislamu ambao wanakutana Jijini hapa kujadili nini kifanyike kuirejesha katika ustaarabu wake.
Wanawake waislamu Jijini hapa wameungana na wenzao wazaliwa wa Tanga wanaoishi Jijini Dar es salaam kuandaa kongamano la kuukaribisha mwezi wa Ramadhani litakalohudhuriwa na Mufti wa Tanzania Sheikh Zuberi Bin Ali Bin Zuberi mgeni rasmi akiwa Mkuu wa mkoa wa Tanga,Balozi Dr Batilda Burian.
Mratibu wa kongamano hilo,Mwanakombo Abdallah amesema kuwa limeandaliwa na kikundi cha Subra na Nusra na litafanyika kesho jumamosi Jijini Tanga.
"Pamoja na kukumbushana wajibu na nafasi ya mwananke katika mwezi mtukufu wa Ramadhani lakini pia kongamano litajadili nini kifanyike kuinusuru jamii na janga kubwa la mmomonyoko wa maadili linalouharibia sifa mkoa wetu wa Tanga"amesema Mwanakombo.
Shamsa Diwani anayeishi Jijini Dar es salaam lakini mzaliwa wa Tanga amesema wamekuwa wakijisikia vibaya wanaposikia matendo yanayofanyika na vijana wa Tanga yakiwamo ya vigodoro na kufanya sherehe ya kupewa talaka kwa sababu si ustaarabu wa mkoa wa Tanga.
"Msituone hivi sisi wazawa wa Tanga tunaoishi mdani na nje ya Tanzania tunajisikia vibaya kusikia matendo mabaya ya kufanya pati ya kupewa talaka na vigodoro yanayofanyika hapa nyumbani...inatuuma na inatutia simanzi kwa sababu si utamaduni wala desturi ya Tanga tumajiuliza ni nani ameleta ushetani huu"amesema Shamsa Diwani.
Hamida Abbas Koja amesema wanazuoni mashuhuri kutoka Mikoa mbalimbali wakiwamo masheikh na masheikhat nchini Tanzania watatoa mada katika kongamano hilo.
"Hili ni kongamano litakuwa ni fursa kwetu ya kujihoji tumekosea wapi na nini kifanyike Ili tuwe katika matendo yenye kumpendezesha Mungu hasa ikizingatiwa kuwa binadamu maisha yetu si lolote si chocolate"amesema Hamida.
MWISHO

No comments:
Post a Comment