DAKTARI HATIANI KUUZA SARUJI NA MATOFALI ZAHANATI SUKURO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 29 March 2026

DAKTARI HATIANI KUUZA SARUJI NA MATOFALI ZAHANATI SUKURO

 

 

Na Mwandishi wetu, Simanjiro


maipacarusha20@gmail.com 


MGANGA mfawidhi wa zahanati ya kijiji cha Sukuro kata ya Komolo wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Dk Daud Ndagala ametiwa hatiani kwa ubadhirifu wa mifuko ya saruji na matofali ya kukarabati zahanati hiyo.


Mahakama ya wilaya ya Simanjiro imemtia hatiani Dk Ndagala kupitia shauri la jinai namba 4344/2026 kwa makosa mawili ya uhujumu uchumi.


Hakimu mkazi mkuu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Simanjiro Charles Uisso amesoma hukumu hiyo Machi 26,2026 na mwendesha mashtaka wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) kituo maalum cha Mirerani Gervas Sarakikiya.


Hakimu Uisso ameieleza mahakama hiyo kuwa Dk Ndagala ametiwa hatiani kwa kufuja Sh1 milioni za mauzo ya mifuko 57 ya saruji ya kukarabati zahanati hiyo.


Amesema pia, Dk Ndagala alichepusha tofali 220 zilizoandaliwa kwa ajili ya ukarabati huo kisha akaziuza Sh605,000 kwa mtu binafsi.


Amesema mshtakiwa huyo amefanya makosa hayo akitumia nafasi yake ya mganga mfawidhi wa zahanati ya Sukuro vibaya kwa dhamana aliyopewa kwa kufanya ubadhirifu.


Amesema mshtakiwa huyo ametiwa hatiani kwa kosa la ubadhirifu wa mali ya umma kinyume na kifungu cha 28 (1) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa na kosa la pili kuchepusha mali kinyume na kifungu cha 29 cha sheria hiyo.


Hata hivyo, hakimu Uisso ameieleza mahakama hiyo kuwa Dk Ndagala amekiri makosa hayo na kufikia makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining) na ofisi ya mkurugenzi wa mashitaka (DPP).


Ameeleza kuwa mahakama hiyo imemuhukumu mshtakiwa huyo kifungo cha nje cha miezi sita na kurejesha fedha zote Sh1.6 milioni kwenye zahanati hiyo ya Sukuro.


Hakimu Uisso amesema hadi wakati wa kusomwa hukumu hiyo mshtakiwa alisharejesha Sh845,000 kwenye akaunti ya zahanati ya Sukuro na kiasi kilichobaki cha Sh843,000 kilipwe kabla ya Julai 26, 2026.


MWISHO

No comments: