Na Julieth Mkireri, MAIPAC Kibaha
maipacarusha20@gmail.com
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kibaha imeadhimisha siku ya Wanawake Duniani huku ikijivunia kuwawezesha wanawake kiuchumi ikiwapambania kuondokana na utegemezi.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo Shukuru Lusanjala amesema Halmashauri hiyo inajivunia kuwawezesha wanawake wengi na wasichana kupitia mikopo ya asilimia kumi.
Lusanjala amesema tangu kurejea utaratibu wa mikopo hiyo tayari wanawake 285 wamenufaika na wengine wataendelea kupata mikopo kulingana na watakavyokuwa wakiomba lengo kuwakwamua kiuchumi.
" Wanawake ndio wenye kubeba majukumu ya kifamilia kwa kuliona hilo Serikali imekuwa ikitoa mikopo ili wanawake ambao hawana uwezo wa kukopa kwenye taasisi nyingine nao waweze kujikwamua kiuchumi," amesema.
Afisa uchaguzi wa Halmashauri hiyo Grace Haule amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyowainua wanawake kupitia nafasi za uongozi.
Pia amewataka wanawake kuwapa kipaumbele watoto wa kike kwenye suala la elimu ili waweze kushika nafasi za uongozi kwenye idara na taasisi mbalimbali.
Zuhura Mteri mmoja wa wanufaika wa mikopo kutoka kundi la wenye ulemavu ameishukuru Halmashauri hiyo kwa kumpatia mkopo ambao umemuondoa kwenye hali ya utegemezi.
Zuhura amesema kuondolewa vikwazo vya kupata mikopo kwa kundi hilo ambalo lilikua haliaminiki kumesababisha walio wengi sasa kuondoka kwenye maisha duni na kujitegemea wenyewe kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Mwisho

No comments:
Post a Comment