Hati ya umiliki ardhi ya mwekezaji aliyedai kuzuia kuingia kwake yasitishwa - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 18 March 2026

Hati ya umiliki ardhi ya mwekezaji aliyedai kuzuia kuingia kwake yasitishwa

 



Mwanasheria wa Kampuni ya Ker & Downey Safaris Limited (KDT), ambayo pia inamilikiwa na mwekezaji kutoka nchini Marekani, Asubuhi Yoyo

Mwandishi wetu,Arusha


maipacarusha20@gmail.com 


Serikali mkoa wa Arusha, imengilia kati Mgogoro  wa umiliki wa ardhi unaowahusisha wawekezaji wa kigeni kutoka nchini Marekani,  katika sekta ya utalii wilayani Arumeru mkoani Arusha kwa kuamua kusitisha hati ya umiliki wa ardhi ekari 10.58  ambayo alipatiwa mwekezaji  George Hurtly wa kampuni ya Kigelia Africana Limited.


Uamuzi huo, umefikiwa baada ya kikao kufanyika baina ya pande mbili zilizopo kwenye mgogoro huo, kwa kusimamiwa na Ofisi ya Kamishna wa ardhi mkoa wa Arusha na baada ya kubainika,hati ya umiliki eneo hilo ilitolewa kimakosa kwa kuwa kuna shauri  juu ya eneo hilo mahakamani.


Hata hivyo, Kamishna wa kazi mkoa wa Arusha, Frank Minzikuntwe  akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, alikiri ofisi yake kuingilia mgogoro huo na kusitisha hati iliyotolewa  baada ya  kufanya vikao na pande zote na jana kutembelea eneo hilo kupitia alama za mipaka ya ardhi.


"Hili jambo kwa sasa ziwezi kulizungumzia mpaka nipate kibali cha Katibu Mkuu, lakini Ofisi ya mkuu wa mkoa itaweza kulitolea ufafanuzi baada ya sisi kukamilisha mchakato wetu wa uchunguzi baada ya leo kutembelea eneo la mgogoro na pia jana kukutana na pande zote"alisema


Akizungumzia mgogoro huo, jana baada ya kukamilika ukaguzi wa mipaka, Mwanasheria wa Kampuni ya Ker & Downey Safaris Limited (KDT), ambayo pia inamilikiwa na mwekezaji kutoka nchini Marekani, Asubuhi Yoyo, alisema kimsingi mgogoro wa eneo hilo, umemalizwa na Kamishna wa ardhi baada ya kubaini, hati ya umiliki wa eneo hilo aliyopewa mwekezaji  George Hurtly wa kampuni ya Kigelia Africana Limited ilitolewa kimakosa.


"Alipewa hati mwezi Februari mwaka huu, baada ya kupeleka taarifa  idara za ardhi, bila kueleza ukweli kuwa kuna mgogoro mahakamani juu ya eneo hili la ekari 10.58 na sasa baada ya hati hiyo  kusitishwa  ina maana mgogoro ulioibuka mwishoni mwa wiki kudai kuzuiwa kuingilia eneo lake umekwisha"alisema


Alisema kilichotokea mwishoni mwa wiki sio, mwekezaji huyo kuzuia kuingia ofisini, bali walinzi wake ndio walizuiwa baada ya kuingilia eneo la KDT na kuanza kujenga uzio kuzuia barabara kutumika wakati akijua eneo hilo sio la kwao.


"Sasa sisi baada ya kuona barabara inafungwa ndipo tulikwenda polisi na kutoa taarifa na polisi walifika na kuwaondoa walinzi wake na pia tayari halmashauri ya Arusha DC ilikuwa imempa barua ya kumtaka kusitisha ujenzi katika eneo hilo"alisema


Alisema kampuni ya KDT ndio ilimuuzia eneo mwekezaji huyo, awali aliuziwa ekari 22 na baadaye alikuwa auziwe heka 10 lakini alikiuka mkataba na ndipo alirudishiwa fedha lakini alikuwa akigomea na kutaka kuendelea na malipo na shauri lipo mahakamani hadi sasa.


"Hapa mwekezaji huyu anahoteli yake hapa hapa katika eneo lingine alilouziwa na KDT  na hakuna ambaye anamzuia kama ambavyo umeona anaingia na kutoka na kilichotokea na taarifa za upotoshwa na taharuki alizotoa kuwa amezuiwa kuingia kwake jambo ambalo sio sahihi"alisema



Alifafanua kuwa Kampuni ya Kigelia, inayomilikiwa na raia huyo wa Marekani, awali iliingia makubaliano na KDT kununua  eneo hilo , lakini kwa masharti kuwa eneo lote la ekari 600 linalomilikiwa na KDT lipimwe kwanza na kugawanywa katika hati ndogo ndogo kabla ya umiliki kuhamishwa rasmi.


“Hata hivyo, hadi sasa zoezi la upimaji halijakamilika, jambo ambalo lilikuwa msingi wa utekelezaji wa makubaliano yale. Kutokana na hali hiyo, upande wa Kigelia ulivunja masharti ya mkataba na kuanza kuchukua hatua za umiliki bila kufuata taratibu za kisheria, ikiwepo pia kufanya biashara ambazo ni kinyume na makubaliano” alisema Wakili Yoyo.


Kwa mujibu wa maelezo yake, kabla ya mgogoro huo,Hurtly aliwahi kuwa mfanyakazi wa KDT kwa muda mrefu na baadaye aliuziwa ekari 22 bila kuwepo kwa mgogoro wowote na katika eneo hilo amejenga hoteli ambayo haina mgogoro wowote.



“Mauziano ya awali ya ekari 22 yalienda vizuri kabisa na hayana mgogoro. Tatizo limejitokeza kwenye makubaliano mapya ya ekari 10 yaliyofanyika mwaka 2023/2024,” alisisitiza.


Wakili huyo alidai kuwa baada ya kuvunjika kwa makubaliano, Kampuni ya KDT ilichukua hatua ya kusitisha mkataba huo na kumrejeshea mnunuzi fedha kiasi cha dola za Marekani 15,000 alizokuwa amelipa kama sehemu ya makubaliano.


Aidha, alieleza kuwa licha ya kurejeshewa fedha hizo, upande wa Kigelia ulidai umiliki wa eneo hilo na kuanza kulichukua kwa nguvu, ikiwa ni pamoja na kujenga uzio na kuonyesha nia ya kuanzisha hifadhi ndogo ya wanyama (zoo) ndani ya eneo hilo.


Mvutano huo ulifikia hatua mpya mwishoni mwa wiki baada ya Kampuni ya Kigelia kuleta walinzi wapya katika eneo hilo, hatua iliyosababisha mgongano na walinzi waliokuwa wakilinda eneo hilo kwa niaba ya KDT tangu mwaka 2009.


Akizungumza na waandishi jana akiwa eneo la mgogoro, Mwekezaji huyo George Hurtly  alisema anaamini serikali itatenda haki baada ya kuingilia mgogoro huo na kufika kupima katika eneo la tukio.


"Mimi sina cha zaidi kusema kwa kuwa sasa shauri hili limefikishwa mahakamani tutaendelea kutafuta haki huko huko"alisema.


Kutokana na mgogoro huo, Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa pia ametoa taarifa kuwa serikali inafatilia mgogoro huo na taarifa zaidi zitatolewa.


MWISHO.

No comments: