Na Mwandishi wetu, Simanjiro
maipacarusha20@gmail.com
KATIBU wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Wambura Igembya ameagiza bibi kizee mwenye umri wa miaka 105, Maria Nongululu mkazi wa kijiji cha Loiborsiret, kurerejeshewa ekari nne za shamba lake alilonyang'anywa na uongozi wa kijiji hicho.
Katibu Wambura ametoa agizo hilo akiwa na sekretarieti ya CCM Wilaya hiyo, Katibu Mwenezi Mosses Makeseni, Katibu wa Wazazi Sasi Mirumbe na Katibu wa UWT Tichomo Sangija, katika ziara ya kuwashukuru kwa kuichagua CCM, kusikiliza kero na kukagua uhai wa chama.
Katibu Wambura akizungumza Kwenye mkutano wa kijiji cha Loiborsiret ametoa agizo la bibi kizee huyo arejeshwe eneo lake kwani ni haki yake.
""Natoa maelekezo nikiwa katibu wa chama, udhibitisho wa eneo lake unajionyesha dhahiri, mama akarudishiwe eneo lake, kuwatumikia wananchi tuache kuwanyanyasa watu, tumechaguliwa ili tuwatumikie," amesema Igembya.
Amesema CCM Wilaya ya Simanjiro, walipokea malalamiko na kero juu ya serikali ya kijiji hicho hivyo wakafika kusikiliza, kuwapa asante kwa kuichagua CCM katika uchaguzi mkuu wa 2025 na kukagua uhai wa chama.
Awali, bibi kizee huyo Maria Nongululu amemlalamikia Mwenyekiti wa kijiji hicho Kimai Saruni kwa kumnyang'anya eneo lake na kutaka kugawa kwa mtu mwingine ili hali ana nyaraka zote za umiliki.
"Shamba hili ni langu zaidi ya miaka 20 iliyopita hata aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji Raphael Matinda yule pale anafahamu ila huyu Mwenyekiti wa sasa anataka kunidhulumu," amesema Maria.
Akizungumza juu ya hilo Mwenyekiti wa kijiji hicho, Kimei amekanusha vikali kutaka kumdhulumu shamba lake bibi kizee huyo hivyo yeye hahusiki.
Kimei amesema hata suala la malalamiko ya wananchi kuwa anauza maeneo ya malisho ya mifugo yaliyopitishwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi siyo sahihi.
Diwani wa kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga (Mardadi) amesema wananchi wa kijiji hicho wanalalamikia ardhi yao kuporwa hasa eneo la malisho hivyo chama kichukue hatua.
"Chama kinabidi kiingilie kati suala hili kwani wanakijiji wa Loiborsiret walishafanya mpango wa matumizi bora ya ardhi ila hivi sasa wanalalalimika kuporwa kwa ardhi yao," amesema Mardadi.
Amesema kilio cha muda mrefu cha wananchi wa kijiji cha Loiborsiret kifikie mwisho kwani jambo hilo la uuzaji wa ardhi wamelalamikia kila mara.
Mkazi mwingine wa kijiji cha Loiborsiret Karakai Barisha amesema Mwenyekiti wa kijiji hicho Kimei na genge la watu wachache wanauza ardhi ya kijiji hicho iliyotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Barisha amesema ni muda sasa wananchi wa eneo hilo wanalalamika na kupinga juu ya uporaji wa ardhi na kuuzwa kiholela na viongozi wa kijiji wakitumia mihutasari ya mwaka 2022.
Amesema mwaka 2019 wananchi kupitia mkutano mkuu wa kijiji cha Loiborsiret walipitisha mpango wa matumizi bora ya ardhi ila hivi sasa maeneo ya malisho ya mifugo inauzwa.
MWISHO


No comments:
Post a Comment