![]() |
| Mbunge wa Vunjo, Enock Koola akizungumza na wakulima wa kahawa kata ya Mwika Kaskazini |
Na Mwandishi wetu, Moshi
maipacarusha20@gmail.com
Moshi. Ziara ya kuhamasisha kilimo cha kahawa katika Jimbo la Vunjo, inayoongozwa na Mbunge wa jimbo hilo, Enock Zadock Koola, imeendelea kushika kasi katika kata mbalimbali, huku mamia ya wakulima wakijitokeza kupata elimu ya mbinu bora za uzalishaji wa zao hilo la kimkakati.
Katika mwendelezo wa ziara hiyo, mbunge huyo leo alitembelea kata za Mwika Kaskazini na Mamba Kaskazini, akiambatana na Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Joachim, pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, ambapo walitoa elimu na hamasa kwa wakulima wa kahawa.
Akizungumza na wananchi, Koola alisisitiza umuhimu wa kufufua na kuimarisha kilimo cha kahawa kama nguzo kuu ya uchumi wa wakazi wa Vunjo.
Alisema ushirikiano kati ya Serikali, viongozi wa kisiasa na wakulima ni msingi muhimu wa kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa kahawa.
“Ni lazima tushirikiane kwa dhati ili kuhakikisha zao letu la kahawa linazalishwa kwa wingi na ubora wa hali ya juu, hali itakayowawezesha wakulima kupata masoko yenye tija,” amesema Koola.
Kwa upande wake, Dk Joachim aliwahimiza wakulima kutumia mbinu za kisasa za kilimo pamoja na kuzingatia ushauri wa wataalamu ili kuongeza tija na kipato chao kupitia zao hilo.
Naye Mnzava alisisitiza umuhimu wa wakulima kujiunga na vyama vya ushirika pamoja na kutumia pembejeo sahihi ili kuongeza ushindani wa kahawa ya Vunjo katika soko la ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya wakulima walioshiriki katika ziara hiyo walipongeza juhudi za mbunge huyo kwa kushirikiana na Serikali katika kuendeleza zao la kahawa, wakisema hatua hiyo itasaidia kukuza uchumi wa kaya na kuchochea maendeleo ya jamii katika jimbo hilo.

No comments:
Post a Comment