Na Mwandishi wetu, Moshi
maipacarusha20@gmail.com
Moshi. Mpango wa kupanda miche 500,000 ya kahawa bora katika Jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro, umeibua tabasamu kwa wakulima wa kahawa wa Jimbo hilo huku vijana wakishauriwa kujihusisha kikamilifu na kilimo hicho ili kuongeza uzalishaji wenye tija.
Hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya kulifufua zao la kahawa ambalo kwa kipindi cha nyuma lilikumbwa na changamoto za kushuka kwa bei, hali iliyosababisha wakulima wengi kukata tamaa na kupunguza uzalishaji.
Akizungumza katika mkutano wa wakulima wa kahawa uliofanyika Marangu Mashariki, Katibu wa Mbunge wa Vunjo, Iddi Mfinanga, alisema juhudi hizo zinalenga kuongeza uzalishaji, kuboresha kipato cha wakulima na kuirejesha kahawa katika nafasi yake ya zao kuu la biashara.
Mfinanga alisisitiza umuhimu wa kizazi cha sasa kujifunza kutoka kwa wakulima wenye uzoefu ili kuhakikisha maarifa ya kilimo cha kahawa hayapotei, bali yanaendelea kunufaisha jamii kwa muda mrefu.
Aidha, aliwahakikishia wakulima kuwa kuna jitihada zinaendelea kuhakikisha wanapata malipo yao wanayodai kupitia vyama vya ushirika (Amcos), jambo litakaloongeza motisha ya kuendelea kulima zao hilo.
Kwa upande wake, Diwani wa eneo hilo, Innocent Shirima, alisema kufufuliwa kwa kilimo cha kahawa kutaleta mageuzi ya kiuchumi kwa wananchi, akibainisha kuwa bei ya sasa ya zao hilo ni ishara nzuri ya fursa iliyopo.
Naye Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Magabu Mongela, alisema tayari maandalizi ya ugawaji wa miche hiyo yamekamilika na zoezi la upandaji litaanza ndani ya msimu huu wa 2025/26. Pia aliwataka wakulima kuondoa miche ya zamani na kupanda mipya ili kupata mavuno bora zaidi.
Mwisho.
| . |



No comments:
Post a Comment