![]() |
Na Lilian Kasenene,Iringa
maipacarusha20@gmail.com
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Heri James, ameahidi kuendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji mkoani hapo, ikiwa ni pamoja na kukubali kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha taarifa za maendeleo kwa ukanda wa Kusini.
Mbali na ahadi hiyo mkuu huyo wa mkoa ametangaza mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii yaliyopo Iringa
Akifungua mkutano wa wadau wa habari,Wahariri na Waandishi wa Habari ulioandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania, MISA-TAN.
James alisema Serikali ya mkoa huo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi.
"Tayari Serikali imeridhia ombi lenu MISA Tanzania la kuanzisha kituo hicho mkoani Iringa na Sasa wasilisheni maombi rasmi ili mchakato wa kuwapatia eneo ili iweze kukamilika haraka,"alisema.
Hatua hiyo ilielezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wananchi, hususan katika sekta za kilimo, Teknolojia,afya, elimu na biashara, ambazo ni mhimili wa uchumi wa ukanda wa Kusini.
Katika hotuba yake, James alitumia fursa hiyo kuitangaza Iringa kama kitovu kipya cha uwekezaji nchini, akieleza kuwa uchumi wa mkoa huo umeongezeka kwa kasi kutoka Sh trilioni 4.5 mwaka 2020 hadi kufikia zaidi ya Sh trilioni 6.3 mwaka 2024.
Alisema ukuaji huo umetokana na jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, misitu, mifugo, viwanda pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya barabara, maji na umeme.
“Tunayo fursa nyingi za uwekezaji, kuanzia kilimo cha umwagiliaji, viwanda vya kusindika mazao, utalii hadi sekta ya misitu. Mkoa wetu uko tayari kupokea wawekezaji,” alisema mkuu huyo wa Mkoa.
Aliongeza kuwa sekta ya kilimo inaendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa mkoa huo kwa kuchangia zaidi ya asilimia 85 ya pato la mkoa na kuajiri zaidi ya asilimia 82 ya wananchi.
Aidha, alisema Serikali imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika huduma za jamii ambapo mabilioni ya shilingi yametumika kuboresha sekta za afya, elimu na maji, hatua inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, upatikanaji wa maji safi umefikia zaidi ya asilimia 80, huku vijiji vyote mkoani humo vikiwa vimeunganishwa na huduma ya umeme, jambo linalorahisisha uwekezaji na shughuli za uzalishaji.
Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, alisema kituo cha taarifa kinachotarajiwa kujengwa kitakuwa jukwaa la kusambaza taarifa muhimu kwa wananchi zikiwemo bei za mazao, hali ya hewa, teknolojia za kilimo pamoja na masuala ya afya na elimu.
Alisema pamoja na hilo, taasisi hiyo inaendelea kuhamasisha uandishi wa habari wenye mwelekeo wa suluhisho ili kusaidia jamii kupata majibu ya changamoto zinazowakabili.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, aliwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kubadili mitazamo ya wananchi, akisisitiza kuwa maendeleo ya nchi yanahitaji mabadiliko ya fikra hasa kwa vijana.
Mkutano huo ulielezwa kuwa ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari na wadau wa maendeleo, huku ukitarajiwa kuchochea uandishi wa habari unaolenga kujenga jamii na kuhamasisha maendeleo endelevu.
Mkutano huo wa wadau wa habari wakiwemo wahariri, na waandishi wa habari ni kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
![]() |
Mwisho.




No comments:
Post a Comment