Na mwandishi Wetu
maipacarusha20@gmail.com
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu mkoa wa Mtwara, imewakumbusha Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria walioko katika Utumishi wa Umma, kuendelea kutoa ushauri wa kisheria kwa Viongozi, Watendaji wa Serikali na Wananchi, na kutoa tafsiri sahihi za sheria kwa Taasisi wanazozihudumia ili kuboresha utawala bora wa sheria.
Wito huo umetolewa na Wakili wa Serikali Mkoa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Nunu Twalib Mangu, wakati akizungumza kwenye kikao cha mawakili wa serikali na Maafisa sharia mkoa wa Mtwara,kilichofanyika leo tarehe 13 machi 2026 Mjini Mtwara.
Akizungumzia nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika serikali, Taasisi za serikali na wanasheria wote katika utumishi wa umma,Wakili Mangu amekumbusha juu ya Uandaaji na Mapitio ya Mikataba ya Serikali, kushauri na kuhakiki mikataba inayohusu Serikali ili kulinda maslahi ya Taifa.
“Ni wajibu wetu kama wanasheria wa Serikali kuhakikisha kuwa tunatekeleza majukumu yetu kwa uadilifu, weledi na uzalendo mkubwa ili kusaidia Serikali kufikia malengo yake ya maendeleo kwa kuzingatia misingi ya sharia” amesisitiza Wakili Mangu.
Akifungua kikao hicho, Wakili wa Serikali Mfawidhi Ofisi ya Wakili mkuu wa Serikali Thomas Muhushi amesema lengo lake ni kuwakutanisha mawakili na maafisa sharia wa serikali mkoa wa mtwara, ili kushirikiana na kujadili masuala mbalimbali yanayohusi utendaji wao wa kazi.
Amewaeleza washiriki kuendeleza ushirikiano katika kutekeleza majukumu kwa viongozi wa serikali, wananchi na wadau wengine katika kutoa ushauri na msaada wa kisheria,elimu ya sharia na umuhimu wa kufuata sharia.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao hicho,Vivian Swai ambaye ni Wakili wa Serikali-Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, amesema kikao hicho ni muhimu katika kukumbusha majukumu na kupeana maelekezo ili kuendelea kuihudumia jamii ya watanzania.



No comments:
Post a Comment