RUZUKU YA BILIONI 5.4 YATOLEWA NA REA KWA MRADI WA UMEME WA MAJI LUPALI NJOMBE - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 12 March 2026

RUZUKU YA BILIONI 5.4 YATOLEWA NA REA KWA MRADI WA UMEME WA MAJI LUPALI NJOMBE

 




Na Lilian Kasenene, Njombe


maipacarusha20@gmail.com


MRADI wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Lupali wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 317, unaotekelezwa na Shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha, umenufaika na ruzuku ya shilingi bilioni 5.4 kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA).


Mradi huo unatumia nguvu ya maporomoko madogo ya maji ya Mto Lupali kuzalisha umeme unaosambazwa katika maeneo ya Mkoa wa Njombe.


Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea mradi huo, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yessaya, alisema Serikali kupitia REA imetoa ruzuku hiyo kwa awamu tano zenye jumla ya shilingi bilioni 5.4.


Alieleza kuwa mradi huo unaotekelezwa na Shirika la Benedictine Sisters of St. Gertrud Convent Imiliwaha una uwezo wa kuzalisha kilowati 317 za umeme.




Aidha, alisema fedha zilizotolewa na REA zimewezesha ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme pamoja na miundombinu ya usambazaji katika kituo cha Imiliwaha Sisters Convent na vijiji jirani vya Boimanda, Kitulila na Matola, sambamba na kuwezesha tafiti mbalimbali za mradi huo.


Kwa sasa, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 99. Kazi zilizotekelezwa hadi sasa ni pamoja na ujenzi wa kizuizi cha maji na mtaro wa kupitisha maji ya mafuriko, ambao tayari umekamilika.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akizungumza kwa niaba ya wahariri waliotembelea mradi huo, alisema wameridhishwa na namna REA inavyotekeleza majukumu yake kwa kutoa ufadhili kwa taasisi mbalimbali.


Alisema uwekezaji wa takribani shilingi bilioni 5.4 katika mradi huo utachangia kuongeza ubora na upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Njombe.


Naye Mratibu wa Mradi huo, Sista Imakulata Mlowe, alisema mara baada ya mradi kukamilika, umeme utakaozalishwa utauzwa moja kwa moja kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ambapo tayari mkataba wa kuuziana umeme umeshasainiwa.


Sista Imakulata aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi kwa matumizi ya nyumbani na biashara, pamoja na kupunguza matumizi ya nishati isiyo rafiki kwa mazingira.


Ziara hiyo ya wahariri mkoani Njombe imelenga kukagua utekelezaji wa miradi ya REA inayotekelezwa mkoani humo, pamoja na kujionea maendeleo ya waendelezaji wadogo wa miradi ya kuzalisha umeme nchini na kujadili changamoto pamoja na ufumbuzi wake.


Mwisho.

No comments: