Na Lilian Kasenene, Njombe
maipacarusha20@gmail.com
MSIMAMIZI wa Miradi ya wakala wa Nishati Vijijini(REA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Danstan Kalugira amesema shilingi bilioni 3.1 tayari zimetolewa na Serikali kupitia REA ili kutekeleza mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji takribani 6 vya wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Mhandisi Kalugira alibainisha hayo wakati akizungumza na wahariri wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kuhusu miradi inayotekelezwa na REA katika wilaya ya Ludewa, walipokuwa katika Kijiji Cha Madunda
Alisema, kupelekwa kwa huduma ya umeme katika maeneo ya vitongoji kunawezesha wananchi waliopo maeneo hayo kupata huduma bora ya nishati ya umeme kwa ajili ya Maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Mhandisi Kalugira alisema kuwa, fedha hizo takribani shilingi bilioni 3.1 zilizotolewa na Serikali kupitia REA ili kutekeleza mradi huo wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 6 vilivyopo katika ukanda wa ziwa Nyasa wilaya ya Ludewa ili wananchi wanufaike na huduma hiyo ya umeme.
"Mradi huu umeanza kutekeleza mwezi Julai 2025, 1hapa wilayani Ludewa, mkandarasi kampuni ya SUMA JKT ndiye anayetekeleza mradi huu mkubwa ambao unatarajiwa kuunganishia wateja wapatao 160 wa awali mara baada ya mradi kuwa umekamilika," alisema Mhandisi Kalugira
Aliongeza kuwa, japokuwa kipindi cha masika mvua nyingi zinanyesha lakini mkandarasi huyo anaendelea kutekeleza mradi kwa kasi, weledi na ni matarajio kuwa atakwenda kumaliza mradi huo kwa wakati katika muda uliopangwa ili wananchi watakaounganishwa na nishati ya umeme waweze kunufaika.
Msimamizi wa kutoka Suma Jkt Yasini Selemanialisema changamoto walizokutana nazo katika mradi huo ni uwepo wa milima,mvua na barabara kuwa mbovu ambapo kwa siku wamekuwa wakivuta nguzo Moja kufika eneo husika kwa kutumia trekta.
"Kwa sasa tunachosubiria ni matilio ili tuweze kuvuta waya,na mpaka sasa tumetumia miezi miwili kusimamisha nguzo 105,na wafanyakazi 80 wote ni kutoka Sumajkt,"alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha ya utekelezaji wa miradi hiyo inayoendelea katika mkoa wa Njombe na maeneo mengine nchini.
"Tumejionea kwa macho yetu namna fedha hizi zinazotolewa na Serikali na jinsi zinavyotekeleza miradi ya kupeleka huduma ya umeme katika wilaya hii ya Ludewa ili wananchi wapate nishati bora ya uhakika,"alisisitiza Balile.
Ziara ya TEF imelenga kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa na REA katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo miradi ya Awamu ya Pili B (HEP 2B) ya kupeleka umeme kwenye vitongoji vipatavyo 9,009.
Mwisho.


No comments:
Post a Comment