Wafanyakazi Mkoa wa Pwani wahimizwa uwajibikaji na maadili kazini - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 4 March 2026

Wafanyakazi Mkoa wa Pwani wahimizwa uwajibikaji na maadili kazini

 




Na Julieth Mkireri, MAIPAC KIBAHA


Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo, Pili Mnyema, amewataka wajumbe wa baraza hilo kujadili ajenda zenye tija kwa wananchi pamoja na kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.


Mnyema ameyasema hayo Machi 3 wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi Mkoa wa Pwani kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kibaha.


Aidha, amesisitiza uwajibikaji, kufanya kazi kwa nidhamu na uadilifu, pamoja na kuhimiza ushirikiano ili kutoa huduma bora kwa wananchi.


“Niwapongeze kwa mafanikio yaliyofikiwa, kwani Mkoa wa Pwani unaongoza katika mambo mengi yaliyoiwezesha kuwa kinara katika sekta mbalimbali. 


Hivyo, niwaombe tuendelee kushirikiana ili kuendeleza mafanikio hayo na kuufanya mkoa wetu kuwa kinara katika kila sekta,” amesema Mnyema.


Katika hatua nyingine, amewataka wajumbe wa baraza hilo kuipa kipaumbele ajenda ya uwekezaji kwa kufanya kazi kwa ushirikiano, akieleza kuwa Mkoa wa Pwani ni mkoa wa kimkakati katika uwekezaji wa viwanda.


Aidha, kikao hicho kilipata fursa ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mpango wa bajeti wa mwaka 2025/2026, pamoja na kupokea na kupitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya mwaka 2026/2027.


 Vilevile, kilifanya uchaguzi wa Katibu na Katibu Msaidizi, ambapo Ramadhani Mwaiganju alichaguliwa kuwa Katibu, huku Mwajuma Mohamed akichaguliwa kuwa Katibu Msaidizi.


Mwisho

No comments: