![]() |
Na Andrea Ngobole, maipac
maipacarusha20@gmail.com
Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) umeiomba Serikali kulinda wanahabari wanapotimiza majukumu Yao ya kutafuta na kutoa habari ili kulinda msingi thabiti wa demokrasia nchini.
Mwenyekiti wa Umoja wa Huo, Ernest Sungura akisoma tamko la taasisi 22 za wanahabari na wadau wa habari wanaounda umoja huo mbele ya waandishi wa habari Leo Aprili 28,2025 jijini Arusha amesema kuwa tathmini ya hivi karibuni inaonesha hali ya uhuru wa vyombo vya habari bado hairidhishi, huku ikizalisha hofu miongoni mwa wanahabari nchini.
Aidha amesema tathmini hiyo imewasilishwa katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yanayoadhimishwa Mei 3, ambapo wadau wa habari wamekuwa wakifanya uchambuzi wa kina kuhusu hali halisi ya tasnia hiyo nchini Tanzania.
Amesema katika kipindi cha miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili mwaka huu, jumla ya matukio nane ya ukiukwaji dhidi ya wanahabari yameripotiwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Manyara, Mbeya na Mwanza.
Miongoni mwa matukio hayo, wanahabari wamekamatwa na kushikiliwa na polisi, wengine wakanyang’anywa vifaa vyao vya kazi, huku tukio moja likihusisha mwanahabari kuitwa kujieleza kuhusu maudhui ya mahojiano aliyofanya.
Amesema chombo kimoja cha habari kilifungiwa kwa siku 90, huku baadhi ya wanahabari waliokamatwa wakiachiliwa kwa dhamana baada ya kupatiwa msaada wa kisheria.
Kwa mujibu wa takwimu, alizosoma zaidi ya matukio 55 ya ukiukwaji dhidi ya wanahabari na vyombo vya habari yameripotiwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita hadi mwaka 2025.
Hata hivyo ameongeza kuwa hali hiyo inaonesha hakuna mabadiliko makubwa ukilinganisha na mwaka uliopita, ambapo matukio ya aina hiyo yaliendelea kuripotiwa katika kipindi kama hiki cha Januari hadi Aprili.
Amesema kuna haja ya kuchukuliwa hatua madhubuti kulinda uhuru wa vyombo vya habari ili kuimarisha demokrasia na haki ya wananchi kupata taarifa sahihi.


No comments:
Post a Comment