Dkt Samia azindua minara 758, kuwanufaisha zaidi ya wananchi milioni nane - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Friday, 10 April 2026

Dkt Samia azindua minara 758, kuwanufaisha zaidi ya wananchi milioni nane

 





Na Mwandishi Wetu 


maipacarusha20@gmail.com 


Zaidi ya wananchi milioni 8.5 hususan wanaoishi mipakani na vijijini, wanatarajiwa kuondolewa changamoto ya mtandao, baada ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kuzindua minara 758 ya mawasiliano iliyojengwa katika maeneo mbalimbali nchini.


Uzinduzi huo umefanyika leo Ijumaa Aprili 10, 2026 jijini Dodoma, ukiambatana na kuunganisha huduma za mkongo wa Taifa wa mawasiliano katika Wilaya 85, ikiwa ni juhudi za Serikali kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuongeza huduma za mawasiliano.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt Samia amesema uwekezaji huo umetokana na ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi kwa ubora unaokidhi mahitaji ya teknolojia ya kisasa na kwa gharama nafuu.


Amesema kukamilika kwa ujenzi wa minara hiyo kutachochea ushiriki wa wananchi katika uchumi wa kidijitali na kufungua fursa mpya za ajira, kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya Taifa.


“Mawasiliano si tena huduma ya anasa kama ilivyokuwa zamani. Leo hii ni uti wa mgongo wa uchumi wa kisasa na daraja la fursa kwa wananchi katika nyanja mbalimbali za maendeleo,” amesema.

No comments: