Makampuni 150 yashiriki MAADHIMISHO ya Wiki ya Usalama Pahala pa Kazi Mkoani Njombe - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Tuesday, 28 April 2026

Makampuni 150 yashiriki MAADHIMISHO ya Wiki ya Usalama Pahala pa Kazi Mkoani Njombe

 

Mkuu wa Mkoa wa Njombe Antony Mtaka Akizungumza katika wiki ya usalama pahsli pa kazi
 



 


Na Mwandishi Wetu


maipacarusha20@gmail.com 


MAADHIMISHO ya Wiki ya Usalama Pahala pa Kazi , yanayofanyika mkoani Njombe, yamefana kwa kushirikisha zaidi ya kampuni 150 hali ambayo imevutia wananchi wengi kuyatembelea.


Maonesho hayo ambayo yameandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi(Osha), yameanza kufanyika Aprili 24,2026  katika viwanja vya Shule ya Msingi Mjimwema.


Akizungumzia mwitikio huo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema unatokana na huduma ambazo zinatolewa katika wiki hiyo.


Amezitaja hizo kuwa ni pamoja na wafanyakazi na wananchi kupima afya na kupata matababu, kupata ushauri wa kisaikolojia na huduma ya afya ya akili.


"Tumekuwa tukifanya maadhimisho haya takribani miaka 20 sasa,ila mwaka huu tumekuja kivingine ambapo mtu akipimwa anapatiwa na matibabu jambo ambalo halikuwepo awali.


"Lakini pia tumekuja na wataalam wengi wakiwemo madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Hospitali ya Afya ya Akili Mirembe na wataalam wengine kutoka Osha na taasisi za vyama vya wafanyakazi," amesema Khadija.


Amesesema maadhimisho yaliyopita ambayo yalifanyika mkoani Singida walifanikiwa kufikia wananchi zaidi ya 3000, lakini mwaka huu matarajio ni kuwafikia 10,000.


Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuzishukuru taasisi na kampuni zilizofadhili, kusaidia wananchi na kushiriki madhimisho hayo wakiwemo Benki ya CRDB, NMB, Kampuni ya Geita Gold Mining, Barick North Mara na wengine.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa, Antony Mtaka amesema maonesho hayo yamekuwa  fursa kwa wakazi wa Njombe ambapo wamefikia hatua ya kuzihama nyumba zao ili wageni wakae kwa kuwakodisha jambo ambalo halijawahi kutokea.


Mataka amesema uwezo wa nyumba za wageni Njombe ni kulaza watu 1800, lakini katika maonesho hayo zaidi ya watu 5000 wamekuja hadi wengine kulazimika kulala Makambako.


"Osha mnaweza kuona maonesho haya  ni jambo la kawaida ila kwetu sisi limegeuka kuwa fursa na kutupa somo la kuongeza nyumba za wageni," amesema.


Amesema wamejiwekea mikakati ya kuufanya mkoa huo kuwa wa kibiashara na kiuchumi  ambapo mwaka huu wamepanga kufanya matukio sita yatakayoleta wageni wengi hivyo kuendelea kuwapa fursa wananchi za kujipatia kipato kwa kutoa huduma kwa wageni watakaofika.

No comments: