![]() |
| WAZIRI Mkuu mstaafu, John Samuel Malecela, |
Na Lilian Kasenene, Same
maipacarusha20@gmail.com
WAZIRI Mkuu mstaafu, John Samuel Malecela, amesema kuwa sekta ya utalii inapaswa kupewa kipaumbele na kuchukuliwa kwa umakini mkubwa, kwani nchi nyingi duniani zinaendesha uchumi wake kupitia mapato ya fedha za kigeni zitokanazo na utalii.
Alisema kuwa katika baadhi ya nchi, serikali zinaendeshwa kwa kiasi kikubwa na mapato ya utalii pekee, hivyo ni muhimu kwa Watanzania kuhakikisha wanadumisha amani na kuonyesha ukarimu kwa wageni wanaotembelea nchi.
Malecela aliyasema hayo wakati akizindua maonesho ya Tamasha la Utalii linalojulikana kama *Same Utalii Festival*, linalofanyika wilayani Same kwa awamu ya tatu sasa.
Alisisitiza kuwa ukarimu kwa watalii ni jambo la msingi sana, akibainisha kuwa baadhi ya maeneo hupoteza fursa za utalii kutokana na kukosekana kwa moyo wa kuwapokea wageni, licha ya mchango wao mkubwa wa fedha za kigeni katika uchumi wa nchi.
Aidha, alisema kuwa mafanikio ya utalii yanategemea sana uwepo wa amani nchini, akiwahimiza Watanzania kuilinda na kuidumisha amani hiyo ili kuvutia watalii wengi zaidi.
> “Katika utalii, ni kama kuwa na kundi la njiwa elfu kumi waliokusanyika sehemu moja; jiwe moja likitupwa, wote hutawanyika. Hivyo, msingi wa utalii wetu uwe ni amani ya nchi yetu,” alisema Malecela.
Pia alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, kwa ubunifu wake wa kuanzisha tamasha hilo, akisema kuwa katika uzoefu wake wa zaidi ya miaka 40 serikalini, hajawahi kushuhudia tukio la aina hiyo likiwavutia watu wengi kutoka maeneo mbalimbali katika ngazi ya wilaya.
“Naomba kusema ukweli, Mkuu wa Wilaya Mungu akuzidishie kwa ubunifu huu. Nimekuwa serikalini kwa zaidi ya miaka 40, lakini sijawahi kuona tukio kama hili likifanyika katika ngazi ya wilaya,” aliongeza.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni, alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa tamasha hilo mwaka 2023, kumekuwa na ongezeko la watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi kutoka watalii 4,000 hadi kufikia 11,000 kwa mwaka. Aidha, katika hifadhi ya Mlima Chome–Shengena, idadi ya watalii imeongezeka kutoka 72 hadi kufikia 200.
Hata hivyo, aliomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuboresha miundombinu katika maeneo ya vivutio ili kuwavutia zaidi watalii, pamoja na kutoa mafunzo kwa waendesha bodaboda ili waweze kuwahudumia na kuwaongoza watalii kwa ufanisi.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mloba Mabula, alisema wizara hiyo itaendelea kushirikiana na Wilaya ya Same kuhakikisha inakuwa mfano wa kuigwa katika kukuza utalii nchini kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea kufanywa.
Mwisho.



No comments:
Post a Comment