Na Mwandishi wetu, Arumeru
maipacarusha20@gmail.com
MWENYEKITI wa chama cha wafanyabishara wa madini Mkoa wa Manyara na kurugenzi ya Habari na Mawasiliano wa chama cha wafanyabishara wa madini Taifa (CHAMMATA) Mokia Ole Mrefu, amewajengea uwezo na kuwapa moyo wanafunzi wa kidato cha sita wa shule ya sekondari Makiba Wilayani Arumeru Mkoani Arusha, wanaotarajia kufanya mtihani wao wa kuhitimu hivi karibuni.
Ole Mrefu amezungumza na wanafunzi hao kwenye maadhimisho ya miaka 30 tangu shule hiyo ianzishwe na mahafali ya 15 ya kidato cha sita kwa kuwatakia kila la heri katika mtihani wao wa kuhitimu.
'Hongereni sana vijana wetu jasiri wa kidato cha sita mnaojiandaa kuhitimu, leo nasimama kuwapa moyo na kuwakumbusha jambo moja muhimu: mmefika hapa si kwa bahati, bali kwa juhudi, nidhamu, na uvumilivu wenu," amesema Ole Mrefu .
Ameeleza kwamba safari waliyoipitia imekuwa na changamoto nyingi, masomo magumu, mitihani ya majaribio, na nyakati za kuchoka, lakini bado mmesimama imara, hiyo peke yake ni ushindi mkubwa.
"Kadri mnavyoelekea kwenye mitihani yenu ya mwisho, kumbukeni kwamba, kujiamini ni silaha yenu kubwa, kila ulichojifunza kina thamani,kila swali lina nafasi ya kujibiwa, msiruhusu hofu iwazuie kung’ara, badala yake, tumieni maarifa yenu, amini uwezo wenu na fanyeni kila mtihani kwa utulivu na umakini," amesema.
"Kumbukeni pia, mitihani hii si mwisho wa maisha bali ni mlango wa mwanzo mpya, mlango wa ndoto zenu, mafanikio yenu, na mchango wenu kwa taifa letu," amesema.
Amewatakia akili tulivu wakati wa mitihani, afya njema na matokeo yenye mafanikio makubwa.
"Nendeni mkang’ae, mkaziwakilishe vyema familia zenu, shule yetu, na Taifa letu, dunia inawasubiri kwa mikono miwili, kila la heri wahitimu wetu, ushindi ni wenu," amesema Ole Mrefu.
Mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite, Bilionea Saniniu Laizer ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo amewatakia kila la heri wahitimu hao wanaotarajiwa kufanya mtihani wao hivi karibuni.
Bilionea Laizer ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu ya jumuiya ya maridhiano Tanzania na Mwenyekiti wa wazee wa jumuiya ya maridhiano Tanzania amesema ana matumaini makubwa kwa vijana hao katika ufaulu wao.
"Ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa kinara wa kujali elimu na mimi nawachangia shilingi milioni nne za kununua mashine ya kudurufu kwa ajili ya shule yenu," ameeleza Bilionea Laizer.
MWISHO

No comments:
Post a Comment