NAIBU WAZIRI WA ELIMU AAGIZA VETA KUANZISHA VITUO VYA UMAHIRI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 26 April 2026

NAIBU WAZIRI WA ELIMU AAGIZA VETA KUANZISHA VITUO VYA UMAHIRI

 




Na Mwandishi Wetu 


maipacarusha20@gmail.com


NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, ameiagiza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) nchini kuangalia uwezekano wa kuanzisha vituo vya umahiri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ili vijana waweze kupata mafunzo ya kisasa yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira.


Agizo hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mtaala mpya wa mafunzo ya ufundi wa aluminium na ufungaji wa vioo (Aluminium and Glass Fitting with Metal Fabrication), ulioandaliwa kupitia ushirikiano kati ya VETA na Aluminium Emirates Profile.


Akizungumza katika hafla hiyo, Wanu alisema elimu ya ufundi inayojikita katika ujuzi wa vitendo ni suluhisho muhimu la changamoto ya ajira kwa vijana nchini. Alieleza kuwa Serikali imejipanga kuimarisha mitaala inayozalisha wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa kwa ufanisi.


Alisema mtaala huo umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya soko la ajira pamoja na mabadiliko ya teknolojia, huku ukitoa kipaumbele kwa mafunzo ya vitendo yatakayowawezesha vijana kufanya kazi kwa ushindani.


“Tunataka vijana wetu wapate ujuzi unaokwenda sambamba na mahitaji ya soko la sasa na teknolojia mpya,” alisema Wanu.


Aliongeza kuwa Serikali imeelekeza kuanzishwa kwa mitaala ya aluminium katika vyuo vya VETA ili kurasimisha na kutambua rasmi ujuzi wa mafundi hao nchini. Alisema wahitimu wa mafunzo hayo watapatiwa vyeti rasmi vitakavyowawezesha kutambulika kitaaluma na kupata ajira kwa urahisi zaidi.


Katika kuhamasisha ushiriki wa vijana, alisema atadhamini vijana 10 kutoka jimbo lake kujiunga na mafunzo hayo, huku akitoa kipaumbele kwa watoto wa kike. Alibainisha kuwa kazi za aluminium na ufungaji vioo zinategemea zaidi matumizi ya teknolojia kuliko nguvu za mwili, hivyo kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume kushiriki.


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Husseni Omar, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za mafunzo na sekta ya viwanda ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi unaohitajika moja kwa moja kazini.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, alisema ushiriki wa mamlaka hiyo katika mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakidhi mahitaji halisi ya soko la ajira.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Aluminium Emirates Profile, Degratius Marandu, alisema ushirikiano huo utawezesha wakufunzi na mafundi kunufaika na maarifa pamoja na teknolojia za kisasa zitakazoongeza ufanisi na ubora katika sekta ya ujenzi nchini.


Mwisho.

No comments: