REA : SH BIL 25 YAJENGA KITUO CHA KUPOZA UMEME IFAKARA, WAIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME UKANDA WA MOROGORO KUSINI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 1 April 2026

REA : SH BIL 25 YAJENGA KITUO CHA KUPOZA UMEME IFAKARA, WAIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME UKANDA WA MOROGORO KUSINI

 




Na Lilian Kasenene, Kilombero 


maipacarusha20@gmail.com 


KUKAMILIKA kwa kituo cha upokea, Kupoza na Kusambaza umeme cha Ifaraka kumewaondolea kero ya umeme kukatika mara kwa mara wananchi wa Wilaya za Kilomber,Ulanga na Malinyi,kilichojengwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini(REA) kwa shilingi bilioni 25.


Hayo yameelezwa wakati wa ziara ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tanzania Editors Forum-TEF) waliotembelea mradi huo wa umeme kujionea utekelezaji wake na tija yake kwa maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Morogoro Kusini.

 

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyoba, akizungumza na wahariri hao alisema uwekezaji huo wa serikali ya awamu ya Sita umeongeza uwezo wa upatikanaji wa umeme kutoka megawati 3 hadi megawati 7,huku kituo hicho kukiwa na ziada ya megawati 11.


Alisema kuimarika kwa huduma ya umeme kumechochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, hususan katika sekta za viwanda, kilimo na huduma za kijamii.


“Kabla ya ujenzi wa kituo tulikuwa tukitumia laini moja ya umeme kutoka Kidatu megawati 3.5 ambapo kulikuwa na changamoto kubwa kutokana na usafirishaji, lakini kwa sasa kero hiyo imeisha baada ya kuzalisha megawati 18 na kati ya hizo ni megawati saba pekee hutumika na zingine 11 hubaki,"alisema Mkuu wa Wilaya ya Kilombero.


Alisema sasa ni wakati wa wawekezaji kuja Ifakara kuwekeza kwani sasa kuna umeme usiokatikakati, na kuna fursa nyingi kutokana na kuwepo kwa umeme wa uhakika.


“Kuna fursa za uwekezaji katika nyanja nyigi kama kwenye uchimbaji madini, utalii katika Hifadhi ya Nyerere, Udzungwa na fursa zingine ni kilimo cha ufuta, viungo, pamba, korosho, miwa na parachichi,” alisema DC Kyoba.


Kwa upande wake, Meneja wa Usimamizi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Deogratius Nagu, alisema gharama za mradi huo zinahusisha pia ujenzi wa njia za kusafirisha umeme za msongo wa kilovolti 33 zenye urefu wa kilometa 70 pamoja na gharama za mshauri elekezi.


Mhandisi Nagu alibainisha kuwa, kituo hicho ni cha kisasa, kikiwa na teknolojia kutoka nchi mbalimbali ikiwemo transfoma kutoka Bulgaria, mifumo ya udhibiti na ulinzi kutoka Hispania pamoja na mifumo ya switching kutoka Ujerumani.


“Kituo hiki kimeondoa changamoto ya upatikanaji wa umeme katika wilaya za Kilombero na Ulanga na kuwezesha wananchi kuendeleza shughuli za uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao,” alisema Nagu.


Naye Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, amesema uwekezaji huo unaonesha matumizi sahihi ya rasilimali za umma na mchango wa REA katika kusambaza huduma ya umeme vijijini.


Ameongeza kuwa ongezeko la matumizi ya umeme linaashiria kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika eneo hilo la Ifakara.


Baadhi ya wanufaika wa mradi huo walieleza namna walivyonufaika na huduma ya umeme wa uhakika.


Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kilimo Ifakara, Setina Ngailo, alisema huduma ya umeme imeimarika na kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme iliyokuwa ikiathiri shughuli za shule.


Naye Msimamizi wa Hospitali ya Kansa ya Good Samaritan, Father Charles Masawe, alisema upatikanaji wa umeme wa uhakika umeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya kwa kupunguza utegemezi wa jenereta.


Meneja wa Kiwanda cha Kukoboa Mpunga cha Bezelengule, Enos Machumu, alisema uzalishaji umeongezeka kwa kiasi kikubwa kufuatia kuboreshwa kwa huduma ya umeme, hali iliyorejesha wateja na kulinda mitambo dhidi ya uharibifu.


Mradi huo umetajwa kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika ukanda wa Morogoro Kusini, huku serikali ikiendelea na juhudi za kusambaza umeme katika vitongoji vilivyobaki ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi wote.

Xxx

Mwisho.

No comments: