Ukoo wa Wasechu, Ugweno wakutana Pasaka kuimarisha maadili kwa vijana wao - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 6 April 2026

Ukoo wa Wasechu, Ugweno wakutana Pasaka kuimarisha maadili kwa vijana wao



Na Mwandishi Wetu, Ugweno


maipacarusha20@gmail.com 


Mwenyekiti wa ukoo wa Wasechu, Herbert Msechu, amesema kuwa familia yao imeweka utaratibu wa kukutana kila kipindi cha Pasaka nyumbani Ugweno kwa lengo la kujadili masuala muhimu yanayohusu familia, hususan malezi na maadili ya vijana katika dunia ya sasa ya utandawazi.


Akizungumza wakati wa ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kifula, Wilaya ya Mwanga, amesema mabadiliko ya teknolojia na kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii yameleta changamoto mpya kwa vijana, hali inayowalazimu wazazi na walezi kuchukua hatua za makusudi kuwajenga watoto katika misingi bora ya maadili.


"Kila pasaka huwa tunafika nyumbani Ugweno kuzungumza mambo yanayotuhusu sisi kama familia, lakini katika maadili ya kujenga vijana wetu ambao sasahivi dunia ulimebadilika imekuwa ni ya kiutandawazi na mambo mengi sana ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mitandao ambao vijana hujifunza moja kwa moja,"


Amesema"Sisi kama familia tumeona kwamba ni vyema tukawa na vijana wetu kuzungumza nao juu ya maadili ili kuepusha yale yanayotokana na mitandao.Kwa mfano,tunajaribu kuelimisha vijana wetu kwamba waepuke sana mambo ambayo yanaenda kinyume na mapenzi ya Mungu na maandiko  yetu ya dini yanavyotuelekeza.


Aliongeza kuwa familia hiyo imekuwa ikiwahimiza vijana wao kuepuka vitendo vinavyokwenda kinyume na mafundisho ya dini, ikiwa ni pamoja na matumizi ya lugha zisizofaa mitandaoni.


"Hivyo sisi kama familia tunatamani sana vijana wetu wasiwe kati ya hao vijana, hivyo tunachokifanya sisi tunatamani vijana wetu hata ingewezekana koo, na makabila mengine katika nchi yetu yakafuata huu mfano. Vijana wakipata misingi mizuri ya maadili kutoka katika familia zao hata haya yanayotokea katika mitandao kinyume kabisa na maadili ya Kitanzania hayajatokea ndio maana vijana wetu tunazungumza nao kipindi kama hiki na tunaona matokeo,"


Akihubiri katika ibada hiyo, Mwinjilisti wa kanisa hilo, Nathaika Msami amesisitiza umuhimu wa usawa katika jamii na imani, akieleza kuwa mshikamano huo ni msingi wa kudumisha maadili na amani katika jamii.


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanaweka na Makundi maalum, Felista Mdemu amesema ipo haja ya kuanzishwa kwa programu maalum za malezi na makuzi ya vijana ili kuwajengea uelewa wa maadili ya kidini na kijamii.


“Tunauomba usharika huu kuweka mikakati madhubuti ya kuwalea vijana wetu ili waweze kuelewa na kuishi katika maadili ya kanisa na jamii kwa ujumla,” amesema Mdemu


Naye, Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mwanga, Joseph Thadayo, amesema  kuwa changamoto kubwa inayokabili jamii kwa sasa ni mmomonyoko wa maadili, akisisitiza wajibu wa wazazi kuhakikisha watoto wanarudi nyumbani wakati wa likizo kushiriki shughuli mbalimbali za kifamilia na kijamii.


“Ni muhimu watoto kushiriki kazi za nyumbani na shughuli za kijamii pamoja na ibada, kwani hilo linawajenga katika misingi bora ya maisha,” amesema Thadayo.


Aliongeza kuwa uzoefu huo husaidia vijana kuwa na uhusiano mzuri na jamii na kuelewa thamani ya familia, tofauti na mazingira ya mijini wanamoishi kwa muda mwingi.


Aidha,  alitoa wito kwa Watanzania kuhakikisha wanadumisha misingi ya maadili kwa vijana ili kujenga taifa bora kwa vizazi vijavyo.


“Ili Tanzania ya miaka 100 ijayo iwe imara, ni lazima tuwajenge vijana wetu katika misingi ya kukumbuka nyumbani, kushiriki maendeleo ya familia na jamii,"amesema Thadayo


Mwisho.

No comments: