Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
WADAU wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT–MMMAM) wamekutana mkoani Morogoro kuandaa mpango kazi wa programu hiyo utakaotumika katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.
Akizungumza katika kikao hicho, Mratibu wa Huduma za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto, Ephrahim Kafilimbi, alisema mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha elimu ya malezi katika ngazi zote za msingi.
Kafilimbi alibainisha hayo wakati akifungua kikao kazi cha siku nne cha wadau wa MMMAM kinachoendelea mkoani Morogoro.
Aidha, alisema mpango huo umelenga pia kuanzisha huduma za kona za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika vituo vya afya na maeneo yote ya kutolea huduma za afya.
Naye Afisa kutoka Taasisi ya Benjamin Mkapa anayesimamia Afua za Kijamii na Watoto, ambao wanafadhili mpango huo, Clarensi Mkoba, alisema taasisi yao kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI watahakikisha mpango huo unatekelezwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Nao baadhi ya wadau wa kikao hicho, akiwemo Mary Shadrack Mtunha ambaye ni Afisa Muuguzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, pamoja na Afisa Lishe Sakina Magadi kutoka mkoa wa Tanga, walisema mpango huo unawasaidia sana katika utekelezaji wa majukumu yao na kwamba mpango kazi unaoandaliwa sasa utakwenda kuboresha zaidi programu hiyo ya MMMAM.
Mafunzo hayo ya siku nne yanahusisha wadau wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto - MMMAM wakiwemo maafisa Ustawi wa Jamii Maafisa Lishe, Waauguzi na Wakunga kutoka Mikoa mbalimbali ya Tanzania.
....



No comments:
Post a Comment