Wanafunzi Mashati Sekondari wabuni utengenezaji sabuni kwa vitendo - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 22 April 2026

Wanafunzi Mashati Sekondari wabuni utengenezaji sabuni kwa vitendo

 




Na Mwandishi Wetu, maipac 


maipacarusha20@gmail.com 


Moshi.Wanafunzi wa kidato cha sita wanaosoma tahasusi ya PMC katika Shule ya Sekondari Mashati, wilayani Rombo, wameonyesha ubunifu kwa kutengeneza sabuni za aina mbalimbali kwa kutumia maarifa waliyojifunza darasani.


Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kuunganisha nadharia na vitendo, ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kukuza ubunifu katika kutatua changamoto za kijamii.


Ubunifu huo umeonyeshwa wakati wa mahafali ya kwanza ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo, ambapo jumla ya wanafunzi 28 wanatarajiwa kuhitimu masomo yao mwaka huu.


Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Abraham Macha alisema wazo la kutengeneza sabuni limetokana na elimu waliyoipata darasani na sasa wamefanikiwa kulitekeleza kwa vitendo.


Alisema tayari wameanzisha mradi uliosaidia shule kupunguza gharama za ununuzi wa sabuni kwa ajili ya usafi, huku pia ukiwapatia kipato wanafunzi hao.


Aidha, alisema wameanzisha kampuni iitwayo Povu, itakayojihusisha na uzalishaji wa sabuni, na kwamba mapato yatakayopatikana yatasaidia kuendeleza mradi huo hata baada ya kuhitimu masomo yao.



Kwa upande wake, mwanafunzi Tawel Manase alisema wanazalisha sabuni za maji, mche na unga, hatua ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji wa shughuli za usafi shuleni hapo.


Aliongeza kuwa hutumia siku za mwishoni mwa wiki kuzalisha sabuni hizo na wanatarajia kupanua zaidi mradi huo kwa kuboresha vifungashio pamoja na utambulisho wa bidhaa zao.


Naye mwanafunzi David Gaudence alisema mradi huo utawasaidia vijana kujitegemea na kupunguza utegemezi kwa wazazi au ajira serikalini baada ya kuhitimu masomo yao.


Akizungumza katika mahafali hayo, Mtendaji Mkuu wa Benki ya Akiba Commercial Bank, Silvest Arumasi, aliwapongeza wanafunzi hao na kuahidi kuwasaidia mtaji ili waendeleze mradi wao.


Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Emmanuel Mrosso, aliishukuru serikali na wadau wa elimu kwa kuendelea kuisaidia shule hiyo katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.


Alisema wanafunzi wanaohitimu mwaka huu ni kundi la kwanza tangu kuanzishwa kwa kidato cha tano mwaka 2024, hatua aliyosema ni ya kihistoria kwa shule hiyo.



Mwisho.

No comments: