Na Mwandishi wetu
maipacarusha20@gmail.com
Imeelezwa kuwa ujio wa michuano ya Afcon 2027 hapa jijini Arusha, utainufaisha moja kwa Moja Kata ya Engutoto na wananchi wake kwa ujumla.
Wakazi wa Engutoto wametakiwa kushiriki Moja kwa moja katika maandalizi ya michuano hiyo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dr Samiah Suluhu Hassan katika kuwasogezea miundombinu ya michezo.
Akizungumza naMaipac media katika mahojiano maalum, Diwani wa Kata ya Engutoto Mh Hamza Njiku ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaletea mradi wa Uwanja wa mazoezi kwa ajili ya michezo ya Afcon katika kata yao.
"Serikali imetuletea mradi wa Uwanja wa mpira wa miguu ambao utatumika kwa ajili ya mazoezi kwa timu za Afcon zitakazotumia Uwanja wa Arusha,Uwanja huo utajengwa katika eneo ilipo Ofisi yetu ya kata jirani na kituo cha polisi cha Engutoto,"alisema Mh Njiku.
Aidha Diwani Njiku amesema Uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki elfu tano waliokaa na utakuwa na maegesho ya kupokea magari mia Tano yakiwemo Mabasi mawili ya timu.
"Uwanja wa Engutoto unajengwa kwa viwango vya Kimataifa vinavyokidhi vigezo vyote vya Afcon,"aliongeza diwani Njiku.
Uwanja wa Engutoto unaogharamiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo unatarajiwa kukamilika mnamo mwezi Oktoba, mwaka huu na tayari mkandarasi ameshapatikana.
Mh Njiku amesema Uwanja wa michezo wa Engutoto utakapokamilika utakabidhiwa kwa Halmashauri ya jiji la Arusha na hiyo itakuwa alama ya kudumu ya michuano ya Afcon 2027 kwa jiji la Arusha na Kata yao.
Amewataka Wana Engutoto kuchangamkia fursa zinazoambatana na ujenzi wa Uwanja huo ikiwemo wauzaji wa Vifaa vya ujenzi,mafundi ujenzi na hata wauzaji vyakula kwa maana ya Baba na Mama Lishe wa kata hiyo.

No comments:
Post a Comment