EKARI 68 ZA BANGI ZATEKETEZWA KWA MOTO TABORA - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 2 May 2026

EKARI 68 ZA BANGI ZATEKETEZWA KWA MOTO TABORA

 




Na Mwandishi Wetu 


maipacarusha20@gmail.com


MAPAMBANO dhidi ya dawa za kulevya nchini yamezidi kushika kasi, huku Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ikiendelea kuonesha dhamira ya dhati katika kutokomeza uhalifu huo, ambapo mkoani Tabora, jumla ya ekari 68 za mashamba ya bangi zimeteketezwa.


Operesheni hiyo maalum iliyofanyika kwa ushirikiano kati ya DCEA, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo, ilihusisha maeneo ya hifadhi ya msitu wa Igombe River wilayani Uyui na hifadhi ya msitu wa Nyahua wilayani Sikonge.


Mbali na kuteketeza mashamba hayo, pia jumla ya gunia 133 za bangi zilikamatwa na watuhumiwa saba kutiwa mbaroni.




Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema kuwa mamlaka hiyo ipo katika operesheni maalum ya kitaifa inayolenga kuteketeza dawa za kulevya zinazozalishwa ndani ya nchi.



Ameeleza kuwa mwelekeo wa sasa umejikita zaidi katika kupambana na uzalishaji wa ndani kufuatia kupungua kwa usafirishaji wa dawa za kulevya kutoka nje ya nchi, hasa zile za viwandani.



 “Kwa sasa tunaelekeza nguvu kubwa katika maeneo ya uzalishaji wa ndani ili kuhakikisha tunadhibiti kabisa tatizo hili kuanzia chanzo chake,” Kamishna Lyimo.




Aidha, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiwezesha DCEA, hususan kwa kuanzisha ofisi za kanda ya Magharibi zenye makao yake mkoani Tabora, hatua aliyosema imeongeza ufanisi wa operesheni na kasi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya.




Kamishna Lyimo ameipongeza uongozi wa Mkoa wa Tabora kwa ushirikiano mkubwa uliowezesha kufanikisha operesheni hiyo, akibainisha kuwa bangi nyingi hulimwa kwa kujificha ndani ya hifadhi na mapori, hali inayohitaji juhudi za pamoja kuikomesha.




“Mamlaka haitavumilia vitendo vya uhalifu vinavyoathiri mustakabali wa taifa. Tutaendelea kufanya operesheni endelevu na kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaohusika na kilimo na uzalishaji wa dawa za kulevya" Kamishna Lyimo.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Paul Chacha, ameipongeza DCEA kwa kazi kubwa wanayoifanya, akisisitiza kuwa mkoa huo utaendelea kushirikiana na vyombo vyote vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha tatizo la bangi linakomeshwa kabisa.


Ametoa agizo kwa askari wa TFS kuweka kambi katika maeneo ya hifadhi na mapori yanayotumika kwa shughuli haramu, ili kudhibiti kikamilifu vitendo vya kilimo cha bangi na kulinda rasilimali za misitu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.


Mwisho.

No comments: