Na Mwandishi wetu
maipacarusha20@gmail.com
Mwenyekiti wa Baraza la madiwani halmashauri ya Meru mkoani Arusha,Lucas Kaaya amewataka viongozi serikali za mitaa wote kwenye kata zote za Meru kuhakikisha wanawapa wananchi elimu ya mikopo inayotolewa na Serikali na kuachana na mikopo ambayo ni hatari
Aidha mwenyekiti huyo alisema kuwa kwa sasa ndani ya baadhi ya kata wananchi wake wamejikuta wakiwa kwenye Hali ngumu ya kiuchumi kutokana na kukopa mikopo hatarishi maarufu kama kausha damu
Mwenyekiti huyo alisema hayo mapema Leo ,May 12 kwenye Baraza la madiwani ambalo limefanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo
Kaaya alisema kuwa mikopo ya Kausha Damu imekuwa ni mwiba sana kwa wananchi na mikopo hiyo imekuwa ikiwatesa wakopaji ikiwa ni pamoja na kuwafilisi kabisa huku Serikali ikiwa na mikopo isiyokuwa na Riba kabisa
Alisema kuwa kinachosababisha wananchi hasa wa kata za ndani kabisa kukimbilia kwenye mikopo hiyo ya Kausha Damu ni kwa kuwa Hawana elimu sahihi ya fursa za mikopo zilizopo
Alifafanua kuwa huu ni wakati sasa wa kila kiongozi wa kata kuhalikisha kuwa anakuwa balozi mzuri wa mikopo ya Halmashauri lakini pia kuwapa faida za mikopo hiyo
"Naelekeza watendaji wote,maafisa Tarafa lakini pia hata ninyi madiwani muhakikishe mnapokutana na wananchi mnawambia uzuri wa mikopo hii ambayo inatolewa Tena kwa wepesi kabisa ,serikali imeamua kuwapa fursa wananchi hiyo fursa sasa inatakiwa iwe faida"aliongeza
Wakati huo huo alisema kuwa kwa sasa zipo baadhi ya Taasisi za mikopo ambazo zimejikita vijiji na vitongoji vya ndani kabisa na havina nyaraka husika za kufanya kazi hiyo ya utoaji wa mikopo hivyo kuanzia sasa Kila kiongozi ahakikishe anafuatilia kwa umakini sana suala Hilo
"Watu wa mikopo ya kausha damu wamekuwa wajanja sana wameamua kuingia ndani ndani huko asilimia kubwa wanawaumiza wananchi wetu kwa kuwa hawana elimu ya fedha ya kutosha lakini pia wanawafilisi bila kufuata taratibu hivyo basi kuanzia sasa nitahakikisha nafuatilia kata kwa kata"aliongeza
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmahauri hiyo Mwalimu Zainabu Makwinya alisema kuwa Hali ya Halmashauri hiyo inaenda vyema ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi
Zainabu alisema kuwa mkakati mbalimbali iliowekwa kwa kiwango kikubwa imefanyiwa kazi ikiwa ni ushirikiano wanaopata baina ya madiwani na wakuu wa idara
Pia alisema kuwa pamoja na hayo Bado anaendelea kutoa wito kwa watendaji wa Kila kata na maafisa Tarafa kuhakikksha kuwa wenyeviti hawabaki na mihuri
Alisema kuwa agizo Hilo ni waraka maalumu kutoka ngazi za juu za uongozi na hivyo basi linatakiwa kuzingatiwa
Akichangia kwenye Baraza Hilo Mmoja wa madiwani kutoka katika kata ya Maroroni,Abrahamu Zelothe(kifaru) alisema kuwa pamoja na kuwa Halmashauri inapambana sana katika kuhakikisha kuwa inaleta maendeleo Bado kwenye kata yake Kuna changamoto lukuki
Abrahamu alisema kuwa changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa umeme katika baadhi ya vitongoji Hali ambayo inafanya baadhi ya maendeleo kuzorota
Alisema kuwa katika vitongoji vya Nazareti,Bondeni,na Samaria wamekosa umeme kabisa Hali ambayo kwa sasa Halmashauri inatakiwa kushugulikia kwa haraka sana
Alisema kuwa umeme una nafasi kubwa sana ya kufuta umaskini hivyo mamlaka husika inatakiwa kuhakikisha kuwa inafuatilia suala Hilo kwa karibu sana
Alihitimisha kwa kusema kuwa hata Hali ya barabara katika kata Hiyo Bado ni mbaya hivyo wakuu wa idara wanaohusika na barabara wanatakiwa kufuatilia suala Hilo kwa ukaribu sana.
Mwisho

No comments:
Post a Comment