Mwandishi Wetu, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imewahimiza Maafisa Ununuzi kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu za ununuzi ili kudhibiti upotevu wa fedha za serikali na kuondoa hoja za ukaguzi zinazojitokeza mara kwa mara katika utekelezaji wa miradi.
Kauli hiyo imetolewa na Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff wakati akifunga mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Vitengo vya Ununuzi TARURA kutoka mikoa yote 26 yaliyofanyika mkoani Morogoro.
Mhandisi Seff alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wataalamu wa ununuzi kuhusu utekelezaji sahihi wa sheria ya ununuzi pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika majukumu yao ya kila siku.
Alisema moja ya changamoto kubwa zinazojitokeza ni kuchaguliwa kwa wakandarasi wasio na uwezo wa kutekeleza miradi kwa ufanisi pamoja na udhaifu katika usimamizi wa dhamana mbalimbali za mikataba, hususan dhamana za malipo ya awali.
"Tumekuwa tukiona changamoto ya dhamana kupita muda wake hususan dhamana za malipo ya awali, hali inayosababisha fedha za serikali kupotea na kuwa vigumu kurejeshwa kutoka kwa wakandarasi waliolipwa", alisema Mhandisi Seff.
Alieleza kuwa kupitia mafunzo hayo wataalamu wamepata nafasi ya kujadili kwa kina changamoto hizo na kukumbushwa wajibu wao wa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa ili kuhakikisha dosari hizo hazijirudii.
Aidha, alisema TARURA imejipanga kuhakikisha hoja zinazohusu dhamana zilizopita muda pamoja na malipo ya awali yasiyorejeshwa hazitaendelea kujitokeza katika taarifa za ukaguzi.
"Tumekubaliana kwamba kuanzia sasa hatutegemei tena kuona hoja za ukaguzi zinazohusu dhamana zilizopita muda au malipo ya awali kutorejeshwa kama inavyotakiwa kimkataba", alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Menejimenti ya Ununuzi TARURA, Bw. Venant Majambo alisema kikao kazi hicho kimelenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa fedha 2025/2026 ambapo zaidi ya asilimia 70 ya fedha zinazotumika TARURA hupitia katika michakato ya ununuzi.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yataisaidia TARURA kuingia katika mwaka mpya wa fedha 2026/2027 ikiwa na wataalamu wenye uelewa mpana wa sheria na taratibu za ununuzi, hatua itakayosaidia kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya fedha za umma.
Bw. Majambo alisema TARURA inalenga kupunguza mapungufu yanayobainishwa katika taarifa za ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), PPRA pamoja na wakaguzi wa ndani kupitia usimamizi madhubuti wa shughuli za ununuzi.



No comments:
Post a Comment