![]() |
| Meneja wa Rasilimali Watu na Utawala wa TCB, Mosses Simwinga akizungumza na Waandishi wa habari Mkoani Kilimanjaro. |
Na Mwandishi wetu, Kilimanjaro
maipacarusha20@gmail.com
Moshi.Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) imewahimiza wakulima wa kahawa nchini, hususan Mkoa wa Kilimanjaro, kuzingatia matumizi ya miche bora na huduma za ugani ili kuongeza uzalishaji na ubora wa zao hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya sherehe za Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi dunia Mei Mosi, zikizofanyika katika uwanja wa chuo kikuu cha Ushirika (MoCu), Meneja wa Rasilimali Watu na Utawala wa TCB, Mosses Simwinga amesema bodi hiyo inaendelea kuhakikisha wakulima wananufaika kwa kupata bei nzuri kupitia upatikanaji wa miche bora na huduma za kitaalamu mashambani.
Amesema TCB kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro imekuwa ikihakikisha taarifa muhimu zinawafikia wakulima kupitia vyama vya ushirika, ili kila mkulima apate miche bora na kupanda katika kipindi sahihi cha mvua.
“Tunawahimiza wakulima wote wa Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo mengine nchini kuhakikisha wanapanda miche bora iliyofanyiwa utafiti na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI),” amesema Simwinga.
Ameongeza kuwa bei ya kahawa imeendelea kuimarika ambapo kahawa inayouzwa kupitia vyama vya ushirika (CPU) imefikia Sh12,000 kwa kilo, huku kahawa ya Arabika inayouzwa majumbani ikifikia Sh9,500 kwa kilo.
Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa wakulima kuuza kahawa yao kupitia mfumo wa vyama vya ushirika ili kupata bei nzuri zaidi na kuongeza ubora wa zao hilo.
“Tunawahimiza wakulima kuhakikisha wanapitisha kahawa yao kwenye mfumo wa CPU ili wanufaike na bei nzuri zaidi. Sisi kama TCB tupo tayari kuwasaidia wakulima popote wanapokwama,” amesema.
Mwisho.


No comments:
Post a Comment