Wapenda michezo na wananchi wa Arusha kwa ujumla,wametakiwa kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dr Samiah Suluhu Hassan,katika maandalizi ya michuano ya Afcon hapo mwakani.
Aidha wananchi wa Arusha wametakiwa kutambua kuwa ni bahati kubwa kwa Mkoa wa Arusha kupata fursa ya kuhodhi michuano hiyo mikubwa kabisa barani Afrika sambamaba na Majiji ya Dar Es Salaam na Zanzibar.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Maipac Media, Katibu wa Chama Cha Soka mkoa wa Arusha Emmanuel Gabriel Antony amesema nafasi kama hii ya kuandaa michezo ya Afcon unakuja baada ya muda mrefu sana.
Amesema akiwa mmoja wa viongozi wa soka mkoani Arusha anajua fika ujio wa Afcon hapa Arusha utaacha faida kubwa za michezo sio katika eneo la miundombinu tu bali hata katika kurejesha hamasa ya soka mkoani Arusha.
"Najua fika kuwa baada ya Afcon kupita Arusha itaachwa na faida kubwa ya Uwanja wa kisasa wa Samia kule Olmot lakini pia Viwanja vya Magereza,Engutoto na Mgambo ambavyo vitatengenezwa kwa ubora wa hali ya juu kwa ajili ya mazoezi kwa timu zitakazotumia kituo cha Arusha,"alisema Antony.
Kuhusu hamasa ya soka mkoani Arusha, Anthony amesema ni wazi kuwa kwa michezo kadhaa itakayochezwa hapa Arusha itachagiza kwa namna moja au nyingine hamasa ya soka mkoani kwetu.
Ametolea mfano wa timu mbili za ligi Kuu ya NBC ambazo zimehamia hapa Arusha kuwa zimeibua hamasa ya wapenda soka mkoani Arusha.
Kuhusu ujio wa wanamichezo nguli wa kimataifa Didier Drogba aliyezichezea Chelsea na Ivory Coast na Rio Ferdinand aliyekipiga na Manchester United na England, amesema ni jambo jema sana na kila mpenda michezo anatakiwa kumuunga mkono Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Paul Makonda kwa juhudi zake za kuitangaza Tanzania katika uga wa michezo kimataifa.
Katika hatua nyingine Antony amesema ARFA wanaendelea kusimamia na kutekeleza program mbalimbali za soka ikiwemo soka la vijana na wasichana ambapo timu kadhaa za wasichana zimekuwa zikifanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

No comments:
Post a Comment