Burhani Yakub, Tanga.
maipacarusha20@gmail.com
Wanawake wa mkoa wa Tanga wamehimizwa kujitokeza kujisajili katika namba ya utambulisho wa mlipakodi ili kupata fursa ya kukopeshwa kwenye vyombo mbalimbali vya fedha.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Tanga,CPA Castro John ametoa taarifa hiyo leo wakati akifungua kongamano la jukwaa la wanawake na kodi lililofanyika Jijini Tanga.
Amesema mwanamke au mwananchi anapokuwa amejisajili na kuwa na TIN namba inamuwezesha kutambulika na vyombo mbalimbali vya fedha na hivyo kujiweka katika fursa nzuri ya kukopesheka.
"Jitokezeni katika ofisi zetu za TRA mjisajili na kuwa na TIN namba...tupo tayari kuwahudumieni hata jumamosi na jumapili hatimaye muwe walipakodi wa TRA"amesema CPA Castro.
Afisa kodi Mkuu wa TRA makao makuu,Charles Mkumbo amesema jukwaa la wanawake na kodi lilizinduliwa rasmi Machi 6 mwaka huu na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda lengo likiwa ni kuwaweka karibu na Mamlaka hiyo na kunufaika na mifumo ya kodi.
"Jukwaa la wanawake na kodi limewekwa ili kuwaweka karibu na Mamlaka ya Mapato Tanzania hatimaye kusikilizwa changamoto zunazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi wa masuala yahusuyo mifumo ya kodi"amesema Mkumbo.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake wajasiliamali TWCC mkoa wa Tanga,Aziza Ramadhani amesema changamoto kubwa inayowakabili wanawake kupitia vikindi vyao ni kucheleweshewa mikopo na inapotolewa huwa ni kidogo ikilinganishwa na fedha iliyoombwa.
"Unaomba mkopo leo unakuja kupewa mwishoni mwa mwakani hapo hata ile biashara uliyoombea inakuwa imeshapotea na ukiomba milioni 100 unapewa milioni moja...hivi ni kweli Kuna lengo la kumuinua kiuchumi mwanamke au kuendelea kumkamdamiza kwenye umasikini?amehoji Aziza.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara wadogo JWT,Mkoa wa Tanga,Ismail Masoud amesema kuna umuhimu wa kushirikiana kikamilifu baina ya maafisa wa TRA na wajasiliamali ili waweze kupata uelewa juu ya kodi hatimaye iwe rafiki.
"Amesema kwa kuwa wajasiliamali wamepangiwa kuchangia asilumia 70 JWT itawafichua baadhi ya watumishi wa TRA wanaokwamisha juhudi za ulipaji kodi kwa kuweka urasimu wakati wa kutoa huduma"amesema Masoud
MWISHO

No comments:
Post a Comment