
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka
NA Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Vijana imewataka vijana kujikita katika kupata ujuzi maalum na wa kisasa, ikiwemo uwezo wa kutoa suluhu kwa changamoto mbalimbali.
Aidha Serikali imeeleza kuwa kwa sasa nchi ina uhitaji wa asilimia 12.6 ya vijana wenye ujuzi wa hali ya juu ili kuongeza thamani na uhitaji huo kwenye taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka alieleza hayo mkoani Morogoro, wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana la Platform Campus Connect Mkoa wa Morogoro lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA).
“Matatizo kila mtu anayajua tunatafuta suluhu, ndiyo maana tunaposema Idea Hub tunataka watu ambao wanakuja na suluhu”
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Japhari Kubecha, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima,
aliwasisitiza vijana wanaopata mikopo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Aliwataka kuhakikisha wanairejesha mikopo hiyo kwa wakati ili fedha hizo ziendelee kuwafikia vijana wengine wenye uhitaji, hatua itakayochochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii.
“Fedha hizi hazina riba unaporudisha unapata nafasi ya mwingine naye kukopa, unapobaki na fedha unahujumu mwingine kukopesheka ili kuweza kujikwamua”alisema.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utawala, Fedha na Mipango katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Amandus Muhairwa, aliwahimiza vijana kulitumia jukwaa hilo kama mwanzo wa kufungua fursa mpya za maendeleo, ubunifu na ushiriki wao katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Jukwaa la Vijana la Platform Campus Connect linatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kujadili fursa, ushiriki na maendeleo ya vijana pamoja na kuimarisha mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
Mwisho.


No comments:
Post a Comment