Na Mwandishi wetu
maipacarusha20@gmail.com
Wizara ya Maliasili na Utalii imejipanga kwa dhati kuhakikisha inaboresha Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka katika bajeti yake ya mwaka 2026/2027 ili kuweza kuhakikisha inatekeleza majukumu yake muhimu ya ufundishaji, utafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu katika masuala ya usimamizi wa wanyamapori na programu nyingine mbalimbali zitolewazo na Chuo.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mh. Ashatu Kijaji(Mb) amesema kuwa Chuo cha Mweka kimekua msingi imara katika kufanya tafiti mbalimbali ambazo zimekua na mchango mkubwa katika upatikanaji wa taarifa muhimu za kufundishia, mbinu za utatuzi wa migongano baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu katika jamii inayozunguka maeneo yanayohifadhiwa pamoja na kupambana na ujangili na kuendeleza shughuli za uhifadhi na utalii nchini.
Mojawapo wa tafiti hizo ni pamoja na utafiti juu ya changamoto za ufanisi wa usimamizi shirikishi wa maeneo ya jumuiya za wanyamapori nchini.
Katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi pamoja na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi, Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori MWEKA kinaendelea na ujenzi wa darasa moja (1), jiko, vyoo na bafu katika eneo la mafunzo kwa vitendo kijiji cha Arash, Tarafa ya Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro.
Chuo pia kimekarabati nyumba tano (5) za watumishi, vyumba vitano (5) vya madarasa, hosteli nne (4) za wanafunzi na ofisi nane (8) za watumishi. Vilevile, Chuo kimefunga meza ishirini (20) na makabati kumi na nane (18) kwenye ofisi za watumishi.
Katika kuboresha mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi, Chuo kiko katika mchakato wa kununua magari matatu (3) aina ya KAMAZ na kuendelea kuboresha huduma ya mtandao wa intaneti kwa wanafunzi na watumishi.
Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Jimbo la Nungwi, Mh. Mdoe Haji Kombo alisema, "Sekta ya utalii inakua kwa kasi na inachochea maendeleo ya vijana. Serikali ianzishe mfuko kwa vijana wanaopenda kuwepo katika sekta ya utalii, mfuko huo utoe unafuu kwa vijana waweze kupata elimu katika masuala ya utalii na ukarimu.”


No comments:
Post a Comment