CCM YAIPONGEZA FRANONE KWA CSR YA ZAHANATI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Thursday, 4 June 2026

CCM YAIPONGEZA FRANONE KWA CSR YA ZAHANATI

 


Na Mwandishi wetu, Mirerani 


maipacarusha20@gmail.com 


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeipongeza kampuni ya Franone Mining & Gem LTD, inayochimba madini ya Tanzanite kitalu C kwa kujenga zahanati ndani ya eneo tengefu la Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kupitia mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSR).


Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Laban Kilongozi akizungumza baada ya kukagua ujenzi unaoendelea wa zahanati hiyo ameipongeza kampuni ya Franone kwa kujitoa kwa ajili ya wachimbaji na wadau wa madini.


Amesema zahanati hiyo ikikamilika itakuwa inatoa huduma za afya kwa wachimbaji na wadau wa madini ya Tanzanite hivyo ni jambo la kiungwana na la kuungwa mkono.


"Nawakupongeza kampuni ya Franone Mining & Gem LTD kwa ujenzi wa zahanati hii, Mkurugenzi Onesmo Mbise hongereni sana, endelea kutoa kwa jamii kwani hautapungukiwa ila utazidi kuongezewa," amesema Kenani.


Hata hivyo, Kenani amewaasa wadau wengine wa madini kuiga mfano kwa kampuni ya Franone Mining LTD,  katika utekelezaji wa CSR kwani ni takwa la kisheria kutoa huduma kwa jamii kupitia miradi ya afya, elimu, maji na mengine.


Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga amesema Serikali itaendelea kuhakikisha maendeleo ya wananchi yanashirikisha wadau wote wa maendeleo, ikiwemo sekta binafsi na kampuni za uchimbaji madini.


RC Sendiga amesema wameendelea kutoa elimu kwa wengine kwani awali walifanya kikao kikubwa na wadau wa madini juu ya kutekeleza uwajibikaji kwa jamii (CSR) kwani baadhi yao wanadhani ni hisani ili hali ni takwa la kisheria.


"Msimamo wetu ni kuwa kila mdau atashiriki katika maendeleo ya jamii kulingana na ukubwa wa shughuli zake na ujenzi wa zahanati hii ni mfano mzuri wa namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na Serikali kuwaletea wananchi huduma muhimu," amesema RC Sendiga.


Meneja Mkuu wa kampuni ya Franone Mining & Gems LTD, Vituz Ndakize, amesema gharama za ujenzi wa zahanati hiyo ulianza Septemba 12, mwaka 2025 ni Sh201,587,000.00 na hadi sasa umefikia asilimia 98, huku ukitarajiwa kukamilika Juni mwaka huu wa 2026.


Vitus ameeleza kuwa zahanati hiyo itawanufaisha zaidi ya wananchi na wadau 16,000 wa eneo la Mirerani ambao kwa muda mrefu walilazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya nje ya eneo hilo.


Amesema zahanati hiyo imejengwa ikiwa na vyumba vya mapokezi, daktari, sindano, kubadilisha mavazi, maabara na ofisi za mapokezi.


"Pia kwenye zahanati hii kutakuwa na vyumba viwili vya wagonjwa wa kupumzika kwa ajili ya uangalizi, vyumba vya chanjo, wajawazito na kutolea dawa," amesema Vitus.


MWISHO

No comments: