ILO YAZINDUA MWONGOZO WA HABARI ZA UHAMAJI; JOWUTA YATIA NENO - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Saturday, 20 June 2026

ILO YAZINDUA MWONGOZO WA HABARI ZA UHAMAJI; JOWUTA YATIA NENO

 


Mjumbe bodi JOWUTA Tausi Mbowe akichangia mada katika warsha ya viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi vya Wanahabari katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki 



Mwenyekiti JOWUTA Mussa Juma


Mwandishi wetu, Mombasa


maipacarusha20@gmail.com 


Shirika la Kimataifa la Kazi Duniani (ILO), limezindua mwongozo wenye kanzi data kwa wanahabari kuandika na kutangaza habari za wahamaji.

 

Mwongozo huo umezinduliwa jana Ijumaa, Juni 20,2026 na Mshauri Mkuu wa Kiufundi kutoka ILO, Charles Autheman katika warsha ya viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi vya Wanahabari katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki inayoendelea Mombasa nchini Kenya.


Akizindua mwongozo huo, Autheman amesema sasa unapatikana katika mtandao wa ILO ukiwa katika lugha ya Kingereza, Kifaransa, Kiarabu na nyinginezo isipokuwa Kiswahili.


Mtaalam huyo amesema bado kuna changamoto katika uandishi wa habari za wahamaji na wakimbizi hivyo ILO imetoa mwongozo huo ili kurahisisha uandishi ikiwamo matumizi ya maneno yasiyo na ukakasi.


Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Mussa Juma ameshauri ILO kuandaa pia mwongozo huo kwa kugha ya Kiswahili kwa kuwa ni lugha ya kimataifa ambayo inakua kwa kasi duniani na kuwafikia watu wengi.


"Tunalifanyia kazi lakini pia Tanzania mnaweza kutafsiri mwongozo huu kwa lugha ya Kiswahili," amesema mtaam huyo akijibu hoja hiyo.


Warsha hiyo imeandaliwa na ILO kwa kushirikiana na Shirikisho la Wanahabari Afrika (FAJ), Shirikisho la Wanahabari Afrika Mashariki (FEAJ) na Chama cha Waandishi nchini Kenya (KUJ) .


Warsha hii ya kikanda imehudhuriwa na viongozi wa vyama na mashirika ya wanahabari kutoka Comoro, Jibuti, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan, Somalia, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda





No comments: