MBUNGE ENOCK KOOLA AENDELEA KUFUNGUA FURSA KWA WANA VUNJO: ZAIDI YA WANANCHI 300 WAPATIWA MAFUNZO MAALUMU YA UFUGAJI WA NG'OMBE WA MAZIWA NA SAMAKI. - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 15 June 2026

MBUNGE ENOCK KOOLA AENDELEA KUFUNGUA FURSA KWA WANA VUNJO: ZAIDI YA WANANCHI 300 WAPATIWA MAFUNZO MAALUMU YA UFUGAJI WA NG'OMBE WA MAZIWA NA SAMAKI.

 

Wananchi wa Jimbo la Vunjo, Wilaya ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro wakipatiwa mafunzo namna bora ya kufuga ng'ombe wa maziwa na Samaki.


Mwandishi wetu, Moshi


maipacarusha20@gmail.com 


Vunjo.Zaidi ya wananchi 250 kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo la Vunjo wamejitokeza na kushiriki mafunzo maalumu ya ufugaji wa kisasa yaliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Enock Zadock Koola.


Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea washiriki uwezo na ujuzi wa kisasa katika sekta ya mifugo na uvuvi ili kuongeza tija, uzalishaji na kipato cha wananchi.


Katika upande wa ufugaji wa mifugo, washiriki walipatiwa elimu kuhusu ufugaji bora wa ng'ombe wa maziwa na nyama, mbinu za kuandaa chakula bora cha mifugo, pamoja na namna ya kutambua na kudhibiti magonjwa mbalimbali yanayoathiri mifugo hiyo.


Aidha, mafunzo hayo yalihusisha pia ufugaji wa samaki ambapo washiriki walipata elimu ya kina kuhusu ufugaji wa samaki aina ya Sato na Kambale, utengenezaji wa chakula cha samaki, pamoja na ujenzi na usimamizi wa mabwawa ya asili na ya kisasa kwa ajili ya kuongeza uzalishaji.


Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, mmoja wa viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mhe. Sebastian Shilangalila alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Mhe. Enock Koola,kwa juhudi zake za kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo hayo muhimu yenye lengo la kukuza uchumi wa wananchi mmoja mmoja kupitia sekta za mifugo na uvuvi.


Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya MIFUGO (LITA) na Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA)walishiriki kikamilifu kutoa mada mbalimbali katika mafunzo. 


Kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Vunjo, Katibu wa Mbunge,  Iddy Mfinanga, aliwasilisha salamu za Mhe. Enock Koola Mbunge wa Jimbo la Vunjo kwa washiriki wote wa semina hiyo. Katika salamu hizo, alieleza kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwawezesha wananchi kupata maarifa na stadi za kisasa zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji, kujiajiri na kuboresha hali zao za maisha.


Aidha, alibainisha kuwa Mhe. Koola ana matarajio makubwa ya kuona washiriki wanatumia maarifa waliyoyapata kuanzisha na kuendeleza miradi ya ufugaji wa kisasa, hatua itakayochangia maendeleo ya familia zao na uchumi wa Jimbo la Vunjo kwa ujumla.


Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi binafsi za Mbunge wa Jimbo la Vunjo Mhe. Enock Zadock Koolabkwa kushirikiana na Serikali, wadau mbalimbali ndani na nje ya Jimbo la Vunjo anazoendelea nazo kuimarisha sekta za uzalishaji na kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia matumizi ya teknolojia na mbinu bora za kisasa, alianza na kampeni ya ufufuaji wa zao la kahawa kwa kugawa bure miche bora zaidi ya laki tatu, ikifuatiwa na kuhamasisha kilimo cha parachichi za kisasa kwa kugawa bure miche bora zaidi ya elfu ishirini na tano, pamoja na mafunzo ya ufugaji nyuki na mazao ya misitu ambapo zaidi ya vijana themanini walinufaika na fursa hiyo na awamu hii ni katika ufugaji wa ng'ombe wa maziwa na samaki ambapo zaidi ya wananchi 300 wameweza kunufaika.


Mwisho.

No comments: