![]() |
| Meya mstaafu Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya akizungumza jatika mkutano wa hadhara Moshi mjini. |
Na mwandishi wetu, Kilimanjaro
maipacarusha20@gmail.com
Moshi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Manispaa ya Moshi kimeiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi kuhusu madai ya uvamizi na uendelezaji wa maeneo ya wazi unaodaiwa kufanywa kinyume na taratibu zilizowekwa.
Wito huo umetolewa leo Juni 20, 2026 na Meya Mstaafu wa Manispaa ya Moshi kupitia Chadema, Raymond Mboya, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Posta mjini Moshi.
![]() |
| Wanachama wa CHADEMA |
Mboya amesema kuwa wakati Chadema ilipokuwa ikiongoza Manispaa ya Moshi, ilisimamia sera ya kulinda maeneo ya wazi kwa kutoruhusu yaendelezwe, ambapo amedai kuwa baadhi ya maeneo hayo kwa sasa yamevamiwa na kujengwa majengo ya biashara na mengine maegesho kinyume na tararibu.
Kwa mujibu wake, hali hiyo imeibua maswali kuhusu mchakato uliotumika kutoa ruhusa za uendelezaji wa maeneo hayo, jambo ambalo linahitaji uchunguzi wa kina ili kubaini kama kulikuwa na ukiukwaji wa sheria au vitendo vya rushwa.
Aidha, amedai kuwa maeneo mengi ya wazi ambayo hayajauzwa yamepangishwa kwa mikataba ya muda mrefu, na kuitaka Takukuru kuchunguza mwenendo huo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Manispaa ya Moshi, Afrikan Mlay, amesema chama hicho kinaendelea kufuatilia kwa karibu matumizi ya rasilimali za umma na kuhakikisha maslahi ya wananchi yanalindwa wakati wote.
Mlay amesema maeneo ya wazi ni mali ya umma ambayo yanapaswa kutumika kwa manufaa ya wananchi wote, hivyo ni muhimu mamlaka husika kutoa ufafanuzi kuhusu mabadiliko ya matumizi ya baadhi ya maeneo hayo.
“Wananchi wana haki ya kujua namna maeneo haya yalivyobadilishwa matumizi na kupewa watu binafsi. Tunataka uwazi na uwajibikaji katika kila hatua iliyofikiwa,” amesema Mlay.
Amesema Chadema itaendelea kushirikiana na wananchi katika kufuatilia masuala ya maendeleo na kusimamia matumizi sahihi ya mali za umma ili kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa zinafuatwa.
Mlay pia amewahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa pale wanapobaini vitendo vinavyohatarisha maslahi ya umma, akisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kulinda rasilimali za taifa.
Mwisho.


No comments:
Post a Comment