![]() |
| Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo |
Na Lilian Kasenene, Morogoro
maipacarusha20@gmail.com
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limewakamata watuhumiwa 132 kwa makosa mbalimbali yakiwemo mauaji, ukatili wa kijinsia, uwindaji haramu, dawa za kulevya aina ya bangi, unyang'anyi, utengenezaji na usambazaji wa pombe haramu pamoja na makosa ya usalama barabarani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Andrew Kantimbo, alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni kutokana na operesheni na doria maalum zilizofanyika kuanzia Mei 15 hadi Juni 10, 2026.
Kamanda huyo alisema huo ni ushirikiano kati ya Jeshi hilo la Polisi na wananchi katika kudhibiti na kuzuia vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Kamanda Kantimbo alisema kati ya watuhumiwa hao,78 walifikishwa mahakamani, ambapo baadhi yao tayari wamepatikana na hatia na kuhukumiwa kwa makosa mbalimbali.
Miongoni mwa waliotiwa hatiani ni Yossam Nyikwa Mkuyu (40), mkazi wa Kijiji cha Mingo wilayani Mvomero, ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki nyara za Serikali kinyume cha sheria.
Aidha,Adam Mlewa Mayengo maarufu kwa jina la "Pengo" alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jelana Mahakama ya Wilaya ya Gairo baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuvunja na kuiba.
Katika mapambano dhidi ya makosa makubwa dhidi ya maisha ya watu, Jeshi la Polisi lilimkamata Paul Gembe maarufu kwa jina la "Sinenepi" (20), mfugaji mkazi wa Negero, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Kitu Bayayi Geleshi (22).
Tukio hilo lilitokea Juni 8, 2026 katika Kijiji na Kata ya Mziha, Tarafa ya Turiani, Wilaya ya Mvomero, ambapo marehemu alidaiwa kupigwa kichwani kwa kitu butu kufuatia ugomvi uliotokana na ulevi kupindukia. Taratibu za kumfikisha mtuhumiwa mahakamani zinaendelea.
Katika operesheni dhidi ya uhalifu wa maliasili zilizofanyika kwa kushirikiana na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi (TANAPA), Polisi walimkamata Bashiri Hamisi Ngagii (32), mkazi wa Goba, Dar es Salaam, pamoja na Ramadhani Sudi (30) na Salum Juma Lukanda (21)kwa tuhuma za uwindaji haramu, ambapo walikutwa na vipande 42 vya nyama ya swala vilivyokauka.
Katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Kamanda Kantimbo amesema watuhumiwa 91 walikamatwa wakiwa na jumla ya kilogramu 69 na gramu 921 za bangi, huku watuhumiwa wengine watatu wakikamatwa na **bunda 83 za mirungi.
Aidha, watuhumiwa 13 walikamatwa wakiwa na lita 185.5 za pombe haramu aina ya gongo** pamoja na chupa 20 za vinywaji bandia vilivyofanana na Smart Gin.
Polisi pia walikamata watuhumiwa waliohusishwa na matukio ya unyang'anyi wa kutumia pikipiki maarufu kama "vishandu".
Kamanda Kantimbo alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu.
Pia alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kudhibiti uhalifu na kuimarisha amani na usalama katika Mkoa wa Morogoro.
Mwisho.

No comments:
Post a Comment