Sarwatt: Wosia Si Uchuro, Ni Suluhisho la Migogoro ya Mirathi - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Sunday, 7 June 2026

Sarwatt: Wosia Si Uchuro, Ni Suluhisho la Migogoro ya Mirathi

 




Mwandishi wetu,  Kilimanjaro


maipacarusha20@gmail.com


Mkurugenzi wa chama cha Wajane Tanzania (TAWIA) Rose Sarwatt, amesema changamoto za mirathi zimekuwa zikisababisha mateso yasiyo ya lazima kwa wajane, huku akisisitiza kuwa kuandika wosia ni njia muhimu ya kuzuia migogoro hiyo.


Ameyasema hayo mkoani Kilimanjaro wakati wa  uzinduzi wa safari ya kupeleka ujumbe wa umuhimu wa kuandika wosia katika kilele cha Mlima Kilimanjaro. Safari ambayo imehusisha wanawake wajane iliyobeba kauli mbiu isemayo, "Andika Wosia Kuepuka Migogoro ya Mirathi."Ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 23 Juni.


“Kwa zaidi ya miaka 10 tumekuwa tukifanya kazi hii na tumeona changamoto kubwa katika kutetea haki za wajane. Migogoro mingi ya mirathi inaweza kuepukika kwa kuandika wosia. Wosia si uchuro, bali ni njia ya kuonesha upendo na kujali familia yako,” amesema.



Sarwatt amesema changamoto kubwa hujitokeza pale mwanaume anapofariki dunia, ambapo mara nyingi mjane hukabiliwa na manyanyaso na kunyimwa haki zake ndani ya familia.


“Mwanamke mjane mara nyingi hukumbana na vikwazo vingi tofauti na mwanaume anayefiwa na mke. Wajane wengi hukosa sauti katika familia na hukumbana na changamoto mbalimbali za kudhulumiwa mali,” ameongeza.


Amesema TAWIA imeanzisha safari maalumu ya kupeleka ujumbe wa umuhimu wa kuandika wosia hadi kilele cha Mlima Kilimanjaro ikiwa sehemu ya kampeni ya kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu utatuzi wa migogoro ya mirathi.


“Tunataka kuonesha kwamba changamoto za mirathi zinaweza kumalizika kabisa iwapo jamii itapata elimu ya kuandika wosia,” amesema.


Akizungumza jijini Moshi, Mjumbe wa Bodi ya TAWIA na Wakili wa Kujitegemea, Harold Sungusia amesema migogoro mingi ya mirathi nchini inatokana na wananchi kutokuandika wosia au kuandika wosia usiofuata taratibu za kisheria.


“Suala la wosia limekuwa changamoto kubwa. Migogoro ya mirathi ni mingi sana hapa nchini, na chanzo chake kikubwa ni watu kutokuandika wosia au kuandika wosia kwa makosa. Wosia ni tamko la mwisho la mtu kuhusu anachotaka kifanyike baada ya kuondoka duniani, ikiwemo mahali pa kuzikwa, namna mali zake zitakavyogawanywa na nani atasimamia mirathi yake,” amesema Sungusia.


Amesema watu wengi huandika wosia lakini kwa makosa yanayosababisha nyaraka hizo kubatilishwa mahakamani na hivyo kuongeza migogoro katika familia.


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu

Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu  amesema serikali inaendelea kuunga mkono juhudi zinazolenga kuwawezesha wajane kiuchumi, kijamii na kisheria.


Amesema Siku ya Wajane Duniani huadhimishwa kila mwaka Juni 23 na kwamba ameshuhudia kesi nyingi za wajane kudhulumiwa mali baada ya vifo vya waume zao.


“Nimekuwa nikishughulikia kesi nyingi za wajane kudhulumiwa mali baada ya waume zao kufariki dunia. Mara nyingi ndugu wa marehemu hujitokeza kutaka kuchukua mali na kuwanyima haki wajane pamoja na watoto wao,” amesema.


Babu amesisitiza kuwa kuandika wosia si ishara ya kujiandaa kufa, bali ni hatua muhimu ya kulinda familia dhidi ya migogoro ya baadaye.


“Wosia si uchuro. Hakuna anayejua siku ya kuondoka duniani. Ni muhimu kuandika wosia ili kuepusha mateso kwa wajane na watoto baada ya kifo cha mzazi au mlezi,” amesema.


Aidha, ametoa wito kwa jamii kukemea tabia ya kudhulumu mali za wajane, akisema mali nyingi hupatikana kwa ushirikiano wa wanandoa na hivyo wajane wanapaswa kulindwa na kupewa haki zao.


Naye, Cedrick Minja  mtoto wa mjane, amesema amejifunza umuhimu wa kuandika wosia baada ya kushuhudia changamoto ambazo mama yake alipitia baada ya kufiwa na baba yake.


“Nimeona changamoto nyingi ambazo mama yangu alipitia baada ya baba kufariki. Uzoefu huo umenifanya kutambua umuhimu wa kuandika wosia ili familia nyingine zisipitie matatizo kama tuliyoyapitia sisi,” 



Mwisho.

No comments: