SERIKALI YATAJA NGUZO TATU ZA KUCHOCHEA UCHUMI, YASISITIZA UMUHIMU WA AMANI NA UTULIVU - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 1 June 2026

SERIKALI YATAJA NGUZO TATU ZA KUCHOCHEA UCHUMI, YASISITIZA UMUHIMU WA AMANI NA UTULIVU

 

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa

Msimamizi wa Mradi kutoka DAWASA aeleza asilimia 50 ya mradi huo imekamilika






Na Lilian Kasenene,Morogoro 


maipacarusha20@gmail.com 


KATIBU Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo na Msemaji mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amewataka Watanzania kuzingatia kwa umakini maeneo yanayoweza kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi. 


Aliyataja maeneo matatu yenye fursa ikiwemo kuajiri watu wengi, mazao yenye uwezo wa kuongezewa thamani na kuuzwa katika masoko ya nje, pamoja na sekta zenye uwezo wa kufungamanishwa na sekta nyingine ili kuongeza tija na mapato.


Alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea eneo la utekelezaji wa Mradi wa Kimkakati katika Bwawa la Kidunda, wilayani Morogoro, mkoani Morogoro mradi unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA). 


“Lazima tuongeze mauzo ya bidhaa zetu nje ya nchi,ili kuuza nje, mazao haya yanapaswa kuongezewa thamani.Bidhaa kama mchele, mahindi, nyama na madini lazima zizalishwe kwa ubora, zifungashwe vizuri na ziwe na sifa zinazokubalika katika masoko ya kimataifa,”alisema Msigwa.


Akizungumzia suala la kufungamanisha sekta mbalimbali, Msigwa alitolea mfano sekta za madini, kilimo, utalii na michezo, akisema ushirikiano kati ya sekta hizo unaweza kuongeza thamani ya uzalishaji na mapato ya taifa.


Aidha, alieleza kuwa Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa maeneo muhimu ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara nchini. Mkoa huo pia una viwanda 63 vikubwa, viwanda vya kati 1,049, viwanda vidogo 3,147 pamoja na wafanyabiashara 15,970. Alisema uwepo wa shughuli hizo za kiuchumi unahitaji mazingira ya amani na utulivu ili kuongeza uzalishaji na mafanikio.


Hata hivyo, Msigwa alisisitiza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hautawezekana bila kuwepo kwa amani na utulivu nchini.


“Kwa sasa nchi ni shwari, amani ipo na Watanzania wanaendelea na shughuli zao kama kawaida. Wananchi wasiwe na hofu. Changamoto zilizopo zinaendelea kutatuliwa.waendelee kupanga na kutekeleza shughuli zao za maendeleo kwa kuwa Tanzania ni nchi salama na tulivu,”alisema.


Aliongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii, huku amani na utulivu vikiwa nguzo muhimu za kufanikisha malengo hayo.


“Tumkatae mtu yeyote mwenye mwelekeo wa kuvuruga amani, mshikamano na umoja wetu. Hakuna nchi inayoweza kuendelea wakati watu wanatishana, wanazuiana kufanya kazi au kusababisha vurugu. Utulivu ni jukumu la kila Mtanzania,” alisisitiza.


Msigwa alisema nchi zilizoendelea zimefanikiwa kutokana na wananchi wake kufanya kazi katika mazingira ya amani na utulivu.


Alionya kuwa hali ya sintofahamu inaweza kuwakatisha tamaa wawekezaji na kusababisha wananchi kupoteza ajira.


Kuhusu upatikanaji wa maji safi, alisema Serikali kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata maji safi na salama kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2050.


Alieleza kuwa bado kuna changamoto ya upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo, hususan Dar es Salaam na Pwani, hasa kipindi cha Oktoba kila mwaka, licha ya uwepo wa vyanzo vya maji vya Ruvu Juu na Ruvu Chini.


Kutokana na changamoto hiyo, alisema Rais *Samia Suluhu Hassan*alielekeza kuanza kwa ujenzi wa Bwawa la Kidunda, mradi ambao hadi sasa umefikia zaidi ya asilimia 50 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni 336 za fedha za ndani.


Msigwa alisema bwawa hilo, linalojengwa na mkandarasi **Sinohydro Corporation Ltd** chini ya usimamizi wa DAWASA, litakuwa na uwezo wa kuzalisha lita bilioni 190 za maji yatakayotumika kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo kusambaza maji safi na salama kwa wakazi wa Dar es Salaam, Pwani na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Morogoro.


Aliongeza kuwa maji hayo pia yatatumika kulinda ikolojia ya eneo la bwawa, kuzalisha megawati 30 za umeme zitakazoingizwa katika Gridi ya Taifa, pamoja na kusaidia uzalishaji wa miwa katika Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi na shughuli nyingine za kilimo.


Msimamizi wa Mradi wa Bwawa la Kidunda,Kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Christian Gava alisema mradi huo umefikia asilimia 50.3 ya utekelezaji, huku kazi zote kubwa za msingi zikiwa zimekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.


Mhandisi Gava alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika Desemba 2026 na kwamba hadi sasa Serikali imeshamlipa mkandarasi zaidi ya shilingi bilioni 132, huku kukiwa hakuna madai yoyote kutoka kwa mkandarasi au mshauri wa mradi.


Aidha, alisema lita milioni 410 za maji zimetengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo katika shamba la miwa la Mkulazi.


“Tumepokea maelekezo kutoka Serikalini na tutayafanyia kazi. Ni wajibu wetu kuhakikisha tunasimamia mradi huu kwa uadilifu kwa sababu fedha zinazotumika ni kodi za wananchi, ambao wana haki ya kujua namna zinavyotumika,”alisema.


Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro(MoroPc),Nickson Mkilanya aliwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kuelimisha na kuhabarisha jamii kuhusu utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo nchini.



Mwisho.

No comments: