Simai: Kuna Yuda Serikalini anakwamisha maendeleo - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Wednesday, 3 June 2026

Simai: Kuna Yuda Serikalini anakwamisha maendeleo

 



Mwandishi Wetu


maipacarusha20@gmail.com 


Mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Simai Mohamed Said, amesema ndani ya Serikali kuna viongozi wanaomsaliti Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na kukwamisha maendeleo ya nchi.


Simai, ameijenga hoja yake hiyo akiwafananisha viongozi wasaliti na Yuda, huku akiwasihi waache kutumia majina ya viongozi wastaafu na kufanya siasa za 2030 mapema, jambo alilosema linalochonganisha na kuharibu utulivu.


Mbunge huyo, ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma leo, Jumanne Juni 2, 2026 alipochangia hoja katika mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2026/27.


Amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, anaongoza Serikali yake na Watanzania kwa upendo na mshikamano, lakini kufanikiwa kwa Taifa wakati mwingine kuna watu wanaotembea kinyume.


“Leo nambatiza mmoja aliyekuwepo ndani ya Serikali, ni Yuda. Nasema hivyo kwanini, sisi tunataka maendeleo ya nchi yetu, kosa la mama (Dkt Samia) ni wapi? Kwa sababu ya kumuamini mtu kumbe ni Yuda,” amehoji.


Amesisitiza kiongozi huyo msaliti ameibuka hadi katika nyumba za ibada akitafuta huruma za watu na kutumia majina ya viongozi wastaafu ilimradi aonyeshe anapendwa.


“Yuda huyu amesaliti ndugu zake, hata ile familia ambayo ilimlea kisiasa. Hawataki kumuona huyu Yuda. Hata huko nyuma amewahi kutajwa ni mzigo, lakini leo mzigo huu tunao ndani ya Serikali,” amesema.


Amesema tayari ameshawaumiza wengi, wengine walikuwa mbele na sasa wako nyuma, wako wafanyabiashara, watendaji ndani ya Serikali, wengine walikatwakatwa na wameathirika na wana msongo wa mawazo.


“Lakini Yuda tumeanza kumuona anaibuka katika nyumba za ibada kutafuta huruma ya wananchi na makundi mbalimbali, lakini nataka niseme, wabunge wenzangu na Serikali tuamkeni.


“Leo anapita akitaka kutuaminisha sisi kwamba Rais Magufuli (hayati John, Rais wa awamu ya tano) alimpenda sana yeye Yuda. Kama alimpenda kweli mbona alimrusha huko nje ya Dunia huko alitupwa, huko alitupwa,” amesema.


Amesema waliompenda hayati Magufuli wanajulikana na hadi sasa wapo, hivyo kiongozi huyo aliyefariki dunia Machi 21, 2021 aachwe apumzike kwa amani kwa kuwa alifanya kazi nzuri.


“Yuda aache kutumia majina ya watu, tuamkeni wabunge na tusiogope, mimi siwezi kutia ulimi wangu puani. Haya maendeleo tunayoyataka lazima tuhakikishe Serikali inapata utulivu, mawaziri wanakuwa na amani na sisi tunaacha kuchonganishwa,” amesema Simai.


Ametaka ujengwe uchumi imara, mawaziri wasimame vema, washauri wa Rais Dkt Samia waifanye kazi yao vizuri bila kuathiriwa na huyo aliyemwita Yuda.

No comments: