TAKUKURU TANGA YAOKOA SH 116.2 MILIONI UJENZI WA SHULE MBILI - MAIPAC MEDIA TANZANIA

Breaking

MAIPAC MEDIA TANZANIA

A Centre for Indigenous and Pastoralists Community Informations




Monday, 8 June 2026

TAKUKURU TANGA YAOKOA SH 116.2 MILIONI UJENZI WA SHULE MBILI

 

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Ramadhani Ndwatah


Burhani Yakub,Tanga.


maipacarusha20@gmail.com 


Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) imeokoa sh 116.2.milioni ambazo zingesababisha miradi ya elimu katika shule mbili za Sekondari zilizopo Wilaya za Muheza na Tanga Jiji kutokamilishwa.


Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Ramadhani Ndwatah amesema hayo leo wakati akiwasilisha kwa waandishi wa habari taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2026.


Amesema katika kipindi hicho Takukuru imewezesha kuokoa hasara ya sh 116,216,506 za  miradi ya ujenzi wa madarasa na vyoo katika shule ya Sekondari Chongoleani na ujenzi wa Sekondari Kwabastola 


Akizungumzia hasara ambayo ilikuwa itokee katika shule ya Sekondari Chongoleani Mkuu huyo amesema Takukuru imeokoa sh 53,816,504 za ujenzi wa madarasa mawili na sh 40,000,000 za vyoo.


"Katika mradi huu Takukuru imewezesha kuanza utekelezaji licha ya kuwa fedha hizi zilishatolewa tangu Machi 4 mwaka 2024 katika ufuatiliaji ilibainika kuwa kwa upande wa madarasa makadirio ya gharama hususani bei za vifaa vya ujenzi yalikuwa chini ya bei halisi ya soko na kupelekea mfumo wa manunuzi wa kielektroniki (NeST) kukataa zabuni zote kutokana na tofauti ya bei"amesema Ndwatah.


Amesema kwa upande wa vyoo hakukuwa na maandalizi ya makadirio ya gharama na hivyo hivyo taratibu za awali za manunuzi hazikuanzishwa kabisa ambapo Takukuru ilichukua hatua kuimarisha uwajibikaji na mradi kwa sasa upo katika hali nzuri.


Kwa upande wa ujenzi wa shule ya Sekondari Kwabastola amesema Takukuru ilisaidia milango kupakwa vanish, kurekebisha mikanda ya gypsum na kununuliwa kwa vitanda 57 vyote vikiwa na thamani ya sh 22,400,000.


Mkuu huyo amesema kwa ujumla katika kipindi hicho Takukuru imeweza kufuatilia matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi 49 ya maendeleo yenye thamani ya sh 506,730,035,914.33 katika sekta ya Afya,Maji,Elimu, Barabara na Utawala.


Katika eneo la uelimishaji umma Ndwatah amesema Takukuru imewafikia wananchi 189,521 katika kipindi hicho njia zikiwa ni pamoja na semina 57,mikutano ya hadhara 28 uimarishaji wa klabu 163 za wapinga rushwa maonesho 10 na vipindi 37 vya radio


      MWISHO

No comments: